Fursa za kusoma bure nje ya nchi zamwagwa

09Mar 2018
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Fursa za kusoma bure nje ya nchi zamwagwa

WIZARA ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki jana ilisema imepokea fursa za ufadhili wa masomo ya muda mfupi na muda mrefu katika kada mbalimbali kutoka nchi saba, ikiwemo China yenye nafasi zaidi ya 80.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ilizitaja nchi nyingine kuwa ni Japan, Jamhuri ya Korea, Misri, Thailand, Denmark na Israel.

Kwa ufadhili wa masomo ya muda mrefu, taarifa ilisema, Serikali ya China imetoa nafasi 80 za ufadhili wa mafunzo kwa ngazi ya Shahada ya Uzamili kwa Watanzania. 

"Kati ya nafasi hizo, 50 zinagharamiwa kwa kila kitu na nafasi 30 hazitagharimiwa kwa kila kitu," taarifa ilisema na kueleza zaidi:

"Vile vile serikali hiyo itatoa nafasi 20 kwa ajili ya kozi za Nishati na Madini."

Mafunzo hayo, taarifa ilisema, yanaratibiwa na Wizara za Elimu, Sayansi na Teknolojia, ya Madini na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

"Pia, Serikali ya China imetoa fursa za ufadhili wa masomo kwa kipindi cha mwaka mmoja kwa ngazi ya Shahada ya Uzamili katika masuala ya Afya ya Jamii kutoka Chuo Kikuu cha Tsinghua, kilichopo Beijing," ilisema taarifa hiyo. 

"Mafunzo haya yanaratibiwa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto."

Taarifa ya wizara hiyo pia ilisema Serikali ya China imetoa fursa ya ufadhili wa mafunzo kuhusu masuala ya Sheria za Kimataifa kutoka Chuo Kikuu cha masuala ya Nje cha Beijing ambayo yanaratibiwa na Wizara ya Mambo ya Ndani na Wizara ya Katiba na Sheria.

Kadhalika, Wizara pia imepokea fursa za ufadhili wa mafunzo kwa ngazi ya Shahada ya Uzamili katika masuala ya Uchumi na Sera kutoka Chuo Kikuu cha Tsukuba kilichopo Japan, ilisema. 

Mafunzo haya yanaratibiwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, taarifa ilisema zaidi.

Katika hatua nyingine, taarifa ilisema, Serikali ya Jamhuri ya Korea imetoa nafasi tatu za fursa za ufadhili wa mafunzo kwa ngazi ya Shahada ya Uzamili katika Taasisi ya Taifa ya Elimu ya Kimataifa iliyopo nchini humo.

"Maombi yatumwe kupitia anuani ifuatayo: www.gradadmission.tshinghua.cn/f/login," ilisema zaidi taarifa hiyo na kwamba mafunzo yanaratibiwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Serikali ya Thailand imetoa ufadhili wa mafunzo ya miaka miwili kwa ngazi ya Shahada ya Uzamili na Diploma kwa Watanzania, wizara ilisema zaidi.

Kutoka Serikali ya Israel, wizara hiyo imepokea mwaliko kwa Watanzania kushiriki mafunzo kwa ngazi ya Shahada ya Uzamili kuhusu Maendeleo ya Mtoto, mwaliko ambao unaratibiwa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto.

Kwa upande wa ufadhili wa masomo ya muda mfupi, Serikali ya Misri imetoa nafasi kwa Watanzania wote katika Sekta ya Teknolojia ya Uchakataji Madini itakayofanyika jijini Cairo kuanzia Machi 18-29, mwaka huu, ilielezwa zaidi.