Fursa za reli ya kisasa zaanikwa

10Dec 2018
Mary Geofrey
DAR ES SALAAM
Nipashe
Fursa za reli ya kisasa zaanikwa

WAKATI mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa ya Standard Gauge Railway (SGR) ukiwa umefika asilimia 47, imeelezwa kuwa utaenda sambamba na kasi ya ukuaji wa viwanda nchini hususan katika mkoa wa Pwani.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa, aliyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu faida za kiuchumi zinazotokana na ujenzi wa reli hiyo, juzi jijini Dar es Salaam.

Kadogosa alisema kwa mkoa wa Pwani wana fursa kubwa ya kuanzisha viwanda vingi kwa sababu reli hiyo itapita katika maeneo yao, hivyo kuwezesha urahisi wa kusafirisha bidhaa.

“Mkoa wa Pwani una fursa kubwa ya kutengeneza viwanda ambavyo bidhaa zake zitatumika kwa shughuli mbalimbali. Sitashangaa kuwa Kibaha inaongoza kwa kuwa na viwanda vikubwa,” alisema Kadogosa.

Alisema kazi inayoendelea ni kusanifu njia zinazopita wanasanifu stesheni, miundominu ya umeme na mawasiliano.

Alisema katika vituo vya reli lazima maisha na shughuli za wananchi ziendelee kama kawaida.

“Duniani kote asilimia 30 hadi 40 ya mapato ya sekta ya reli hayatokani na uendeshaji wa reli, hivyo ndiyo sababu ya kuwekeza kwenye miradi mikubwa nje ya reli kama viwanda na vituo vya uwekezaji katika stesheni zote,” alisema.

Alisema pia vituo hivyo vitajengwa kwa malengo ya kuhudumia watu wataoatumia mradi huo kwa miaka zaidi ya 100 ijayo.

Alisema pia wameshazungumza na Waziri wa Ardhi, Nyumba na  Maendeleo ya Makazi kwa ajili ya upimaji wa ardhi na watu wa Kibaha wameshaelezwa wajiandae kupima viwanja na maeneo yao tayari kwa shughuli za uwekezaji hususan maeneo zinapojengwa stesheni.

“Hili ni jambo zuri sana, natamani lingeanza miaka 50 iliyopita kwa sababu kwanza utazuia uvamizi uliopo sasa kwenye maeneo ya reli, lakini tukiwa na mpangilio unaoonyesha hii ni njia ya reli ina maana watu hawataingia kwenye njia ya reli,” alisema.

Alisema pia reli hiyo itatumia umeme jambo litakalowezesha fedha nyingi kwenda Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), badala ya kutumika kuagiza mafuta nje.

Alisema pia wanapotumia nishati ya umeme ni rahisi mara tatu ya gharama za kuagiza mafuta kwa sababu zinatumiwa na wenye viwanda na watumiaji wa kawaida.

Kadogosa alisema pia wafanyabiashara wa malori wataendelea kunufaika na biashara kwa sababu watachukua mizigo kuanzia stesheni ya reli kupeleka maeneo mengine.

Alisema treni itatembea kilometa 160 kwa saa, hivyo safari ya kutoka Dodoma hadi Dar es Salaam inaweza kwenda na kurudi zaidi ya mara tatu kwa siku.

“Reli itabadilisha namna tunavyoishi, lakini pia itaongeza mwingiliano wa watu baina ya mkoa mmoja na mwingine,” alisema.

Alisema pia mwongoza treni anaweza kuona njia yote ya treni akiwa Dar es Salaam na kuziongoza vyema.

Alisema mwongozaji anaweza kuziruhusu treni nne kwa wakati mmoja na isilete madhara wala mwingiliano.

“Kwa sasa uendeshaji hatumuachii dereva, mtu anaweza kuisimamisha akiwa sehemu yoyote ile na hii inapunguza gharama za uendeshaji,” alisema.

Alisema reli hizo za kwenda mikoa mbalimbali nchini pamoja na zile zitakazotoa huduma katika Jiji la Dar es Salaam ikiwamo Bagamoyo, Mbagala na uwanja wa ndege zitatoa huduma ili kwendana na kasi ya ongezeko la watu katika jiji hilo wanaotarajiwa kufika milioni 25 ifikapo 2050.

Utekelezaji wa mradi wa kiwango cha kimataifa unaogharimu Sh. trilioni 7.1 utaunganisha mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Kigoma, Katavi na nchi zisizokuwa na Pwani za bandari za Rwanda, Burundi, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Habari Kubwa