Gambo awaahidi wenye ulemavu viti mwendo 100

30Nov 2020
Cynthia Mwilolezi
ARUSHA
Nipashe
Gambo awaahidi wenye ulemavu viti mwendo 100

MBUNGE wa Arusha Mjini, Mrisho Gambo amesema atahakikisha watu wote  wenye ulemavu 565  katika Jiji la Arusha  atawapatia viti mwendo 100 na kuwapatia matibabu kwa kupindi cha miaka mitano kupitia Mfuko wa  Bima ya Afya (NHIF).

Mbunge wa Arusha mjini Mrisho Gambo akizungumza na waandshii wa habari jijini Arusha Leo kuhusu kuanzaa rasmi kwa utekelezaji wa ahadi alizoahidi wakati wa kampenii jijini humo. PICHA:GETRUDE MPEZYA

Aidha amesema atachimba visima vya maji kwenye Soko Kuu la Arusha, Samunge, Kijenge na kwa kuanza ameshachimba kisima katika Soko la Kilombero.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo,Gambo alisema mbali na masoko hayo pia atachimba visima kwenye shule zenye uhitaji wa maji ili wanafunzi wapate huduma hiyo bila kuhangaika.

"Lakini katika uongozi wangu nitaweka nguvu kubwa katika kutatua kero za wafanyakazi wa viwandani na kwa kuanza nitafanya ziara ya siku nne kwenye kiwanda cha A to Z, Sunflug, Lothia na Tanfoam na nitaongozana na wataalamu toka idara ya kazi, Osha, NSSF, PSSF, Mfuko wa Fidia kwa wafanyaka pamoja na viongozi wa vyama vya wafanyakazi,"amesema Gambo.

Amesema ziara hiyo imetokana na kupokea malalamiko mengi ya wafanyakazi hao wakati alipotembelea kwenye viwanda hivyo kuomba kura wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu na kuahidi kuzifanyia kazi mara baada ya kuchaguliwa.

Kwa mujibu wa Gambo, waajiri wengi hawatoi mikataba kwa wafanyakazi wao,lakini viongozi wa serikali wanapowatembelea huonyeshwa mikataba hewa,huku wafanyakazi wakiendelea kuteseka jambo ambalo hakubaliani nalo na atalipigia kelele.

Habari Kubwa