Gambo ataka Ma DC kumpa takwimu wazazi walioshindwa kuwahudumia watoto

12Dec 2019
Allan lsack
ARUSHA
Nipashe
Gambo ataka Ma DC kumpa takwimu wazazi walioshindwa kuwahudumia watoto

MKUU wa Mkoa  wa Arusha Mrisho Gambo, amewaagiza wakuu wa Wilaya kumpelekea takwimu halisi ya wazazi walioshindwa kutimiza wajibu wao wa kuwasomesha na kuwahudumia watoto wao.

MKUU wa Mkoa  wa Arusha Mrisho Gambo.

Agizo hilo, alilitoa juzi wakati wa kilele cha maadhimisho ya siku ya 16 za za kupinga ukatili wa kijinsia.

Licha ya kutoa agizo hilo, Gambo amewataka wakuu wa Wilaya mkoani humo,kutoa taarifa ya matukio ya ukatili wa kijinsia yaliyoripotiwa kwenye Wilaya zao.

Alisema katika taarifa zao, zionyeshe hatua gani zilizochukuliwa,mashauri yaliyopelekwa mahakamani,na ambayo hayakupelekwa na vikwazo walivyokumbana navyo.

Hata hivyo,amewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi na wanasheria wanaoandaa mashtaka kwa ajili ya kupeleka shauri mahakamani.

“Kumekuwepo na tatizo kwa wananchi kutokutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi na wanasheria wanaondaa mashtaka, nawaomba wananchi wote tushirikiane kukabiliana na suala la ukatili wa kijinsia kwa watoto na wanawake,”alisema Gambo.

Pia alisema kikwazo kingine kimekuwa kwa watoa taarifa kuogopa kwenda mahakamani kutoa ushaidi.

“Naomba wananchi wenye nia ya kupambana na matukio haya kuwa tayari kutoa ushirikiano kwa mamlaka husika,”aliema Gambo.

Aidha aliagiza jeshi la polisi kitengo cha dawati la jinsia kuwatafuta wazazi ambao hawatekelezi wajibu wao wa kusomesha watoto na kuwahudumia.

“Wapo Watoto  na wanawake wanaoingia katika matatizo mbalimba baada ya kukosa malezi kutoka kwa Baba nawaume zao,”aliongeza Gambo.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha Jonathan Shana, alisema jeshi hilo, limejipanga kuanzisha msako wa nyumba kwa nyumba  kuwatafuta watu wanaojihusisha na ukatili wa kijinsia.

“Tumejipanga kupambana na wahalifu wanaojihusisha na ukatili wa kijinsia katika Mkoa wa Arusha,”alisema Shana.

Mganga Mfawidhi wa Hosipitali ya Mkoa ya Mount Meru,Shafii Msechu, alisema hospitali hiyo, ina kituo maalumu cha kupokea wahanga  wa ukatili wa kijinsia , kituo hicho kimefungulia mwezi mei mwaka huu.

Alisema tangu kufungulia ka kituo hicho, kimewapokea wahanga 333, na kesi zilizofikishwa mahakamani ni kumi na tisa zipo polisi kwa ajili ya upelelezi zaidi.

Katika kilele cha maadhimiho ya siku ya kupinga ukatili wa kijinsia kitengo cha wananwake cha jeshi la polisi cha kupinga ukatili wa kijinsia kiliwatembelea wahanga katika hospitali ya Mount Meru na kutoa msahada wa sabuni,kanga,maji ya kunywa na juisi kama ishara ya kupinga matukio hayo kwenye jamii.

Habari Kubwa