GGML yadhamini maonyesho ya madini kwa mil. 200/-

19Sep 2020
Na Mwandishi Wetu
Geita
Nipashe
GGML yadhamini maonyesho ya madini kwa mil. 200/-

KAMPUNI ya Geita Gold Mining Limited (GGML), imedhamini Maonyesho ya Tatu ya Teknolojia za Uchimbaji Madini mkoani Geita kwa gharama ya Sh.milioni 200.

Maonyesho hayo yalianza juzi hadi Septemba 27, mwaka huu, huku GGML ikiwa mdhamini mkuu .

Udhamini huo unahusisha gharama za kusawazisha eneo la maonyesho pamoja na kugharamia mabanda 100 pamoja na umeme wa dharura (jenereta na mafuta yake) katika kipindi chote cha maonyesho hayo.

Maonyesho hayo ambayo yanafanyika katika viwanja vya Mamlaka ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji na Mauzo Nje ya Nchi (EPZA) Mjini Geita ambalo pia limejengwa na Kampuni ya GGML kupitia mpango wake wa huduma kwa jamii kwa gharama za Sh. milioni 800.

“GGML inajivunia kudhamini maonyesho haya kwa mwaka wa tatu mfululizo. Mwaka huu tunakusudia kutoa uzoefu wetu wa matumizi ya vifaa mbalimbali vya uchimbaji kwa kampuni nyengine, lakini pia kwa wachimbaji wadogo. Ni jambo zuri pia kwamba tumetoa udhamini huu tukiwa tunaadhimisha miaka 20 ya uwekezaji wetu mkoani Geita na Tanzania.

Tunajivunia kuendeleza ushirikiano na jamii inayotuzunguka kunufaisha wafanyabiashara wa ndani wanaokusudia kufanya kazi na sisi,” alisema Simon Shayo, Makamu wa Rais wa GGML anayeshughulikia miradi endelevu.

“Tunafarijika sana kuona ndoto ya kuwa na kituo cha uwekezaji na biashara ya nje hapa Geita inatimia na GGML inakuwa sehemu ya mafanikio hayo kupitia mpango wake wa kusaidia jamii,” alisema.

Maonyesho haya yanakutanisha kampuni za uchimbaji madini, wachimbaji wadogo na wa kati, wawekezaji na wafanyabiashara kutoka Tanzania na nchi nyingine kwa ajili ya kuonyesha teknolojia zinazotumika katika sekta ya uchimbaji madini na fursa za uwekezaji na biashara kwenye sekta hiyo.

Mwaka 2019, Kamati ya Maandalizi ya Maonyesho ya Teknolojia za Uchimbaji Madini, iliitunukia GGML tuzo ya mshindi wa kwanza aliyetoa elimu na mafunzo ya teknolojia muhimu kwa wachimbaji wadogo sanjari na mifumo ya usalama na uokoaji inayopaswa kutumika migodini.

Habari Kubwa