Gharama matibabu Ndugai yazua jambo

06Jul 2019
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe
Gharama matibabu Ndugai yazua jambo

BARAZA la Wazee wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wamedai wamemwibukia spika wa Bunge, Job Ndugai, huku wakitaka ripoti ya gharama za matibabu ya kiongozi huyo wa chombo cha kutunga sheria alipokuwa India, iwasilishwe bungeni.

Mwenyekiti wa Baraza hilo, Hashim Issa.

Mwenyekiti wa Baraza hilo, Hashim Issa, aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari huku akidai kuwa ndani ya matibabu hayo kuna harufu ya ufisadi.

Issa alidai kuwa matibabu ya Spika Ndugai yalitumia dola za kimarekani milioni 12 na kwamba huo ni ufisadi uliolenga kuvusha fedha ambazo ni kodi za Watanzania.

“Tunataka kuona ripoti zote zinawasilishwa bungeni, vikiwamo vyeti vya matibabu na  madaktari walifanya operesheni,” alisema.

Alidai kuwa Spika Ndugai alikwenda nchini India kutibiwa ingawa hawajui alikuwa anasumbuliwa na nini.

“Matokeo yake alivyorudi Tanzania akasema ametumia Dola za kimarekani milioni 12. Maradhi gani hayo? Kafanya operesheni ngapi? Alikwenda hospitali ya aina gani mpaka alipe dola milioni 12. Hakuna duniani, huo ni ufisadi.

“Hiyo ilikuwa njia ya kuvusha fedha ambazo ni kodi za Watanzania kutumia kisingizio cha maradhi kwenda hospitali, kumbe kavusha fedha,” alidai huku akisisitiza  Baraza la Wazee Chadema, linataka kuona ripoti zote zinawasilishwa bungeni.

“Ripoti ya Spika Ndugai, tunataka vyeti vyote vya hospitali, hesabu ya madaktari, alifanyiwa operesheni ngapi. Tunataka hesabu kamili ya miezi yote ya matibabu kama zimefika Dola za kimarekani milioni 12,” alisema.

Aprili 14, mwaka huu, Spika Ndugai akijibu swali la gharama ya matibabu yake nje ya nchi wakati akizungumza na waandishi wa habari, alisema kuugua kwake kumelisababishia taifa fedha nyingi, hawezi kujua.

“Labda ningekufa watu wangefurahi. Katika matibabu yoyote yale, tunawatibu watu hatuangalii thamani ya mtu na kiwango cha fedha kilichotumika. Kinachoangaliwa  kama kuna matumizi mabaya ndani ya matumizi hayo,” alisema.

“Nilitibiwa mwaka 2015/16 na hesabu hizo ni za 2017/18. Unajua tena mtu akibanwa anatafuta sababu huku na kule. Wanaotibiwa ni wengi na hospitali niliyokwenda kutibiwa ni ya kawaida. Nilikutana na Watanzania wa kila aina, wa aina zote, tunapishana huyu anakwenda kwa daktari huyu, mwingine huyu, sijawahi kwenda hospitali ya New York (Marekani), Ujerumani, naenda India ambako ndiko Watanzania wanakotibiwa,” aliongeza.

Aprili, mwaka jana, Spika Ndugai alirejea nchini akitokea India alikokuwa akipatiwa matibabu ya maradhi yaliyokuwa yakimsumbua kwa miezi kadhaa.