Giza nene mradi stendi ya Mwenge

24Oct 2021
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe Jumapili
Giza nene mradi stendi ya Mwenge

GIZA nene limeendelea kutawala kuhusu maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa kituo kipya cha daladala Mwenge uliosimamishwa Juni 20, mwaka huu.

Wakati bado taarifa ya timu ya uchunguzi wa mradi wa huo haijatoka, viongozi mbalimbali waliotafutwa na Nipashe Jumapili kuzungumzia suala hilo kuanzia ngazi ya wilaya hadi taifa, hawajatoa ushirikiano.

Timu ya uchunguzi ilipewa wiki mbili kuanzia Juni 20, mwaka huu kukamilisha kazi hiyo na kumkabidhi Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Ummy Mwalimu.

Timu hiyo ilipaswa kukamilisha kazi yake Julai 4, mwaka huu, lakini leo hii inatimu miezi mitatu kamili hakuna taarifa yoyote iliyotolewa na ujenzi umesimama kwa miezi minne sasa.

Nipashe ilimfuata Waziri Ummy akiwa mjini Bagamoyo Julai 18, mwaka huu kusaka mustakabali wa mradi huo, akijibu kuwa anakwenda Dodoma na kwamba Juni 19, mwaka huu alitarajia kupata mrejesho wa kamati na kuahidi kutoa majibu ya maswali atakapofika huko makao makuu ya nchi.

Tangu wiki iliyopita, Nipashe Jumapili imekuwa ikiwafuata viongozi mbalimbali wa Wilaya ya Kinondoni na Mkoa wa Dar es Salaam wakiwamo, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Godwin Gondwe na Mkuu wa Mkoa, Amos Makalla, ambao kwa nyakati tofauti walisita kuzungumzia suala hilo, wakiomba wapewe muda zaidi.

Nipashe ilimpigia simu Waziri Ummy jana mchana bila mafanikio na hata ilipomtumia ujumbe mfupi wa maandishi (SMS) kujua kinachoendelea kuhusu mradi huo, hakujibu chochote.

Juni 20, mwaka huu, Waziri Ummy alizuru kwenye mradi huo na kueleza kutoridhishwa na kusuasua kwake na kuweka wazi kwamba amekuwa akipokea malalamiko mengi kutoka kwa wanachi.

“Huu mradi ulipaswa kukamilika Mei 2, mwaka huu lakini hadi sasa ni Juni na ujenzi wake umefikia asilimia 46, nasimamisha ujenzi wake kuanzia sasa na kuunda timu ya kuchunguza,” alisema Ummy siku hiyo.

Waziri huyo alimwagiza Katibu Mkuu TAMISEMI kuunda timu hiyo haraka na kuitaka ifanye kazi katika kipindi cha wiki mbili, ikichunguza pia miradi miwili ambayo ni ya ujenzi wa Uwanja wa Mpira wa Manispaa ya Kinondoni na ujenzi wa jengo la utawala la Manispaa ya Kinondoni.

Mbali na hilo, Waziri Ummy pia alitangaza kumsimamisha kazi Mhandisi wa Manispaa ya Kinondoni, Isaak Mpaki, kutokana na kushindwa kuishauri vizuri Manispaa ya Kinondoni juu ya ujenzi wa miradi hiyo mitatu.

“Kuna figisu kwenye hii miradi, miradi haikamiliki, kila mtu anasema la kwake, huu mradi (stendi ya daladala) ungekamilika ungeingiza faida ya Sh. milioni 480 kwa mwaka, tungejenga shule, hospitali, lakini hadi sasa hakuna kitu," alisema.

Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Spora Liana, alisema siku hiyo kuwa gharama ya ujenzi wa mradi huo ni Sh. bilioni 4.898 na kwamba mkandarasi (361 JWT Lugalo) alikabidhiwa mradi Julai 27 mwaka jana.

Alisema ilipofika Mei 2, mwaka huu ujenzi wa mradi huo ulifikia asilimia 46, hadi siku hiyo Sh. bilioni 1.558 zilikuwa zimeshatumika.

“Changamoto kubwa ni vifaa kutoagizwa kwa wakati, vibarua wachache, ambapo mkandarasi badala ya kutumia askari anaajiri raia, pamoja na kuchelewa kulipwa mishahara yao na kuja ofisi kwangu kunilalamikia,” alisema Liana.

Mkandarasi wa mradi huo, Luteni Kanali David Luoga, alisema Aprili, mwaka jana walianza kazi ya ujenzi wa stendi hiyo na kazi yao ni kujenga lakini vifaa vya ujenzi vinaletwa na Manispaa ya Kinondoni.

“Ilipofika Julai mwaka jana, mtiririko wa vifaa haukuwa mzuri, vikawa vinakuja kwa kusuasua, ilipofika Septemba tuliandika barua ya kuomba vifaa vyote vinavyovihitaji kufika eneo la mradi lakini hadi sasa havijafika,” alisema Luteni Kanali Luoga.

Habari Kubwa