Gondwe aagiza vijiji kufanya mikutano kila Ijumaa

22Mar 2019
Dege Masoli
Handeni
Nipashe
Gondwe aagiza vijiji kufanya mikutano kila Ijumaa

MKUU wa Wilaya ya Handeni, Gondwin Gondwe, ametaka mikutano mikuu ya serikali za vijiji kufanyika siku moja wilaya nzima kila Ijumaa ya wiki ya kwanza.

MKUU wa Wilaya ya Handeni, Gondwin Gondwe, picha mtandao

Aidha, ametishia kuwafikisha kwenye Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (Takukuru) viongozi wote wasiofuata miongozo, kanuni na taratibu za fedha ili kulinda uwajibikaji na matumizi mabaya ya mali za umma.

Gondwe aliyasema hayo wakati wa mkutano wa wadau wa elimu wilayani hapa ambao uliandaliwa na asasi isiyo ya kiserikali ya Tree of Hope ya nchini na kufanyika mjini Handeni kwa ufadhiliwa na Shirika la Foundation for Civil Society.

Alisema suala la serikali za vijiji kutoitisha mikutano mikuu kwa mujibu wa kalenda limekuwa changamoto kubwa kwa viongozi wengi na kulalamikiwa na wananchi.

Alisema kalenda aliyoitangaza ndiyo itakuwa mwarobaini kwa viongozi wasiowajibika na kwamba yeye na maofisa wake watafanya ziara za kushtukiza katika vijiji kufuata kalenda hiyo ili kubaini watakaokaidi agizo hilo.

Kwa upande wa miongozo ya fedha, Gondwe alisema atawapeleka Takukuru viongozi ambao hawatafuata taratibu, kanuni na sheria za fedha na kwamba lengo ni kulinda uwajibikaji na kutaka kufuta matumizi mabaya ya rasilimali za umma.

Awali Mratibu wa mradi huo wa uhamasisha uwajibikaji wa jamii na mamlaka zinazohusika katika kuboresha huduma za elimu, Goodluck Malilo, kwenye taarifa yake ya robo ya pili ya kuanzia Februari hadi Machi 2019, alisema vijiji vinne vilifanyiwa madodoso na kubaini udhaifu kwa baadhi ya viongozi katika uwajibikaji.

Kwa mujibu wa Malilo, maeneo yaliyofanyiwa madodoso na asasi hiyo ni ya vijiji vya Kwedizinga, Michungwani, Kabuku nje na Komsanga na yalifanyika mazungumzo na wadau mbalimbali na kubaini kasoro hizo.

Alitaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni kukosekana uwiano wa ruzuku kwa mwanafunzi wa shule za msingi na baadhi ya walimu kutotambua kiwango halisi cha ruzuku cha kila mwanafunzi na hivyo kushindwa kutoa majibu sahihi yanapotokea malalamiko.

Kasoro nyingine ni kutobandikwa kwenye mbao za matangazo fedha za ruzuku zinazotolewa na serikali katika shule, matumizi ya ruzuku yasiyozingatia miongozo iliyopo, upatikanaji wa fedha usiozingatia uhitaji na matarajio na viongozi wa vijiji kutokuwa na uwazi na uwajibikaji.

Habari Kubwa