Gwajima aagiza uongozi Hospitali zote kuunda kamati kufuatilia mapato

28Nov 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Gwajima aagiza uongozi Hospitali zote kuunda kamati kufuatilia mapato

WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Dorothy Gwajima, amewaagiza viongozi wa Hospitali zote ngazi ya Taifa, Mkoa, Wilaya kuunda Kamati ndogo za ufuatiliaji wa mapato ya fedha za uchangiaji kila siku toka vitengo vyote ili kufahamu bayana kiasi kinachokusanywa-

WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Dorothy Gwajima.

-kwa kuwa imebainika kuna vitengo ambavyo makusanyo yake ya fedha za uchangiaji ni madogo kuliko kilichochangiwa au kilichotarajiwa kuchangiwa.

Dk. Gwajima ametoa maagizo hayo leo Novemba 28, mwaka huu wakati akizungumza na watumishi wa Hospitali ya Rufaa Mkoa Kitete Mjini Tabora ambapo amesema kuwa iundwe Kamati hiyo ndogo ya kusimamia mapato ya fedha ili kudhibiti upotevu wa fedha za umma na utumiaji wa kiasi kidogo cha fedha za uchangiaji kwenye kununua bidhaa afya ikiwemo dawa.

Ameelekeza Kamati hizo pia zihusike na kuchambua iwapo matumizi ya kwenye eneo la dawa na vipimo au bidhaa za afya kiwango kinafikia asilimia 50 au zaidi kama ilivyoelekezwa kwenye mwongozo wa wizara.

Aidha, Dk Gwajima amesema usimamizi mzuri wa uendeshaji wa vituo kwa ujumla wake pamoja na usimamizi mzuri wa uwajibikaji kwenye matumizi ya raslimali zote ikiwemo fedha ni muhimu na ni chachu katika kuboresha huduma na kuvutia wateja wa makundi yote ya uchangiaji huduma ili dhana ya uendelevu wa huduma kwa uchangiaji hususani Bima za Afya itimie kwa ukamilifu wake.

Habari Kubwa