Gwajima alaani mtoto kuuawa kwa maji moto

24Apr 2022
Marco Maduhu
Shinyanga
Nipashe Jumapili
Gwajima alaani mtoto kuuawa kwa maji moto

​​​​​​​WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk. Dorothy Gwajima, amelaani tukio la mtoto Joseph Juma (4) kuuawa na bibi yake, Tatu Moshi (45) kwa kumwagiwa maji ya moto.

​​​​​​​Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk. Dorothy Gwajima.

Waziri Gwajima alitoa kauli hiyo jana alipofanya ziara mkoani hapa na kutembelea kaburi alilozikwa mtoto huyo nyumbani kwao katika Kijiji cha Lyabukande.

Alisema amelazimika kufanya ziara hiyo mkoani Shinyanga, baada ya kusikia tukio hilo la kuuawa kwa mtoto huyo pamoja na mdogo wake Limmy Lameck (1) kujeruhiwa kwa kipigo na bibi yao.

Waziri Gwajima aliitaka jamii inapoona au kusikia mtoto wa jirani anafanyiwa vitendo vya ukatili, kutoa taarifa haraka ili kudhibiti matukio hayo.

Alisema Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009 iliyofanyiwa marekebisho (2019) inakataza mzazi kumuadhibu mtoto na kumsababishia madhara kwenye mwili wake.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Sophia Mjema, alisema katika uchunguzi walioufanya walibaini watoto hao walikuwa wakifungiwa ndani kila siku, wakati bibi na mama yao wanapokwenda kutafuta riziki, lakini majirani walikuwa hawatoi taarifa.

Alisema Serikali mkoani humo wanafanya utaratibu wa kutafuta mlezi ambaye atamlea mtoto huyo kwa muda, wakati mama yake akiendelea kushikiliwa na Jeshi la Polisi, huku bibi yao akishtakiwa kwa tuhuma za mauaji.

Ofisa Maendeleo ya Jamii mkoani Shinyanga, Tedson Ngwale alisema kuanzia mwaka 2021 hadi Machi 2022, matukio ya ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto yaliyoripotiwa yalikuwa 3,288.

Tukio hilo la mauaji ya mtoto huyo pamoja na mdogo wake kujeruhiwa kwa kipigo na bibi yao, lilitokea Aprili 18, mwaka huu majira ya saa 11 alfajiri.

Baada ya tukio hilo, bibi huyo anashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga pamoja na mama yao, Helena Nicolaus.

Habari Kubwa