Gwajima 'aliamsha' Kawe

06Sep 2020
Thobias Mwanakatwe
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Gwajima 'aliamsha' Kawe

WAKATI kampeni zikiendelea kupamba moto, mgombea ubunge wa Kawe (CCM), Askofu Josephat Gwajima, ameahidi kununua greda na maroli kwa fedha zake ili kutengeneza barabara za mitaa yote ya jimbo hilo ikiwa atashinda katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Pia, amesema atanunua magari ya wagonjwa na kuyasambaza jimboni ndani ya siku 90 baada ya kuchaguliwa, akitamba kuwa hahitaji kusubiri bajeti ya serikali.

Askofu Gwajima alitoa ahadi hizo juzi wakati akizungumza na wanachama wa CCM na wananchi wa Kata ya Kawe alikokuwa anaendelea na mikutano yake ya kampeni.

"Mimi sijaja kufanya kazi hii kuganga njaa, acha hao wa upande ule ambao wanaomba ubunge kutumia fedha waliyokopa benki halafu baada ya miaka mitano wanaanza kurejesha marejesho na mpaka amalize marejesho atakuwa hana muda wa kukuletea maendeleo. Mimi sina marejesho ya kurejesha," alitamba.

Askofu Gwajima aliahidi kuwa baada ya kununua greda na maroli hayo ambayo yatatoa ajira kwa vijana wa Jimbo la Kawe, atahakikisha kila barabara ya mtaa inafanyiwa matengenezo na hivyo kumaliza tatizo la barabara katika jimbo lote.

Mgombea huyo aliahidi kununua magari ya wagonjwa kwa ajili ya jimbo hilo, akidai kuwa hata kabla hajawa mbunge, wapo rafiki zake ambao ni wabunge aliwasaidia kununua magari 18, hivyo kwa Jimbo la Kawe, ununuzi wa magari hayo ni jambo dogo sana kwake.

Askofu Gwajima alisema kabla hajafikiria hata kugombea ubunge, alishasaidia watu zaidi 250 na misikiti saba kwa kuwaunganishia maji katika eneo la Salasala kwa gharama zake.

Askofu Gwajima alisema yeye kugombea ubunge kupitia CCM hakujatokea kwa ajili ya kuuza sura wala kuchoma mahindi, bali ni kwa ajili ya kufanya kazi za kuwaletea maendeleo ya kweli wananchi.

Habari Kubwa