Gwajima awafariji waathirika volcano

29Nov 2020
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Gwajima awafariji waathirika volcano

MBUNGE wa Kawe, Josephat Gwajima, amewataka wakazi wa Kunduchi Mtongani ambao nyumba zao zimeathirika na tope la volcano kuwa watulivu, wakati serikali ikiendelea kutafuta namna ya kuwasaidia.

Alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam wakati akikagua makazi ya wananchi yaliyoathirika na tope la volcano eneo la Kunduchi Mtongani.

Akiwa eneo hilo, Gwanjima aliwataka wananchi hao kutoa ushirikiano kwa serikali ikiwamo kufuata maelekezo yanayotolewa ili kuepuka madhara ambayo yanaweza kutokea baadaye.

“Kuwahamishia watu mahali lazima tujue watalala wapi, watakula nini, ukimpa mtu kiwanja bado hujamsaidia, tusikilize kwanza maelezo ya serikali halafu mimi kama mbunge nitashirikiana na nyinyi, bila shaka ndani ya wiki hii, ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, itasema neno,” alisema Gwajima.

Aidha, Gwajima aliahidi kuwa katika hatua yoyote ambayo itachukuliwa na serikali, atahakikisha kila mwananchi anapata haki kutokana na tathmini itakayokuwa imechukuliwa.

“Nawapa pole sana kwa tukio hili ambalo limewapata, kama mwananchi mwenzenu na mwakilishi wenu nitafuatilia jambo hili kwa ukaribu sana, hakuna nyumba wala mtu ambaye ataonewa au kupunjwa kwa namna yoyote ile,” alisema Gwajima.

Mmoja wa wakazi wa eneo hilo,  Salome Mwapili, alisema tatizo la kutokea volcano katika eneo hilo lilianza miaka mitano iliyopita, kwamba lilianza kama kichuguu cha kawaida kabla ya kutoa ufa, kupasuka na baadaye kuanza kutoa kokoto, kisha matope mazito.

“Mvua ikinyesha, maji yanaingia ndani sababu ya hili tope maji yanakosa mahali pakwenda, lakini pia kuna chemchem isiyoisha, kwakweli hali siyo nzuri kama unavyoona,” alisema Mwapili.

Mkazi mwingine wa eneo hilo, Rashidi Aboubakar alisema kutokana na athari hizo, shughuli nyingi za maendeleo zimesimama ikiwamo ujenzi, pamoja na huduma ya za kijamii.

Novemba 22, mwaka huu, Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Aboubakar kunenge, alitembelea eneo la Kunduchi Mtongani ili kutathmini athari zilizojitokeza, kwamba aliwataka wakazi hao kuhama ili kuepuka madhara ambayo yanaweza kutokea, kuahidi kuwa serikali itagawa viwanja vipya eneo lingine.

Habari Kubwa