Hadhi ya Mlima Kilimanjaro kurudishwa

08Jun 2021
Jenifer Gilla
KILIMANJARO
Nipashe
Hadhi ya Mlima Kilimanjaro kurudishwa
  • KINAPA: Tumedhamiria kurudisha uoto wa asili

Jana katika sehemu ya kwanza tulielezea jinsi majanga ya moto yanayoathiri Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro, leo katika sehemu ya pili tunawaletea jinsi KINAPA ikishirikiana na wadau wengine wa hifadhi hiyo wanavyopambana kukabiliana na janga hili pamoja na mengine yanayosababisha kupungua kwa....

Bwalo la kulia chakula katika Shule ya Sekondari Korikie, iliyoko Kitongoji cha Mamba, ni moja ya miradi iliyojengwa na KINAPA, kuhamasisha utunzaji wa mazingira ya hifadhi ya Mlima Kilimanjaro.

miti ya asili.

NI siku ya jumatatu asubuhi, anga imetawaliwa na ukungu, baridi ikipenya kwenye ngozi, lakini kwa namna ya aina yake ni  hali hewa inayoleta raha inayojitegemea.

Hapo ndipo mbele yangu, nipo ana kwa ana na mwenyeji wangu, mzee Imani Kikoti,  Ofisa Uhifadhi Mkuu anayesimamia Idara ya Sayansi na Uhifadhi katika mamlaka ya hifadhi ya Mlima Kilimanjaro (KINAPA).

Sihitaji ushahidi kuthibitisha namna anavyohuzunika utajiri nakshi ya Mlima Kilimanjaro  unavyosambaratishwa na mazingira.

Hapo ndipo ugeni wake wa Nipashe , ukapatwa na hisi ya kumdadisi nini mahususi kinamgusa?

Mzee Kikoti, anaianza sehemu yetu ya pili ya simulizi kwa kwa kauli ifuatayo;

“Zamani ilikuwa ukitoka hapo nje ya geti letu kwenye hicho kijiji  na kutaka kitanda cha mbao inayotokana na mti wowote (mninga,mvule,mkongo), ilikuwa rahisi kupata, lakini sasa hali ni tofauti, vitanda hivyo havipatikani tena maeneo haya”.

Ni maelezo ambayo yanabeba sehemu ya picha ya kilio cha kitaifa namna utajiri wa kimazingira na kiuchumi wa dunia uliobahatika kuwapo nchini ulihujumiwa, lakini kina mzee Kikoti na wadau wengine watetezi wa mlima huo wamefanikisha kudhibiti.

Walivyoshtuka

Mzee Kikoti anasimulia kwamba kwa uzoefu wa macho yao, mara moja walianza kuona uhusiano uliokuwapo kati  kupungua kwa miti katika hifadhi hiyo na  athari zinazoikumba.

Anasimulia, ushuhuda mwingine ukazidi kuwafungua macho,  pasipo kuhitaji darasa la mazingira kwamba barafu ambazo miaka nenda rudi hazikuwa zikiyeyuka, sasa ni mithili ya friji ya barafu ambayo umeme wake umekatwa kwa muda mrefu.

“Mpaka hivi sasa theluji zimefikia kilometa za mraba 1.76, kikubwa ni ongezeko la joto ulimwenguni, kadiri siku zinavyoongeeka joto linaongezeka na barafu zinayeyuka” .

“Japokuwa mabadiliko ya tabia nchi yameuathiri mlima huu lakini kupungua kwa miti nako ‘kumeongeza msumari kwenye kidonda’ kwa sababu hakuna oksijeni ya kutosha kupambana na kaboni inayosababisha ongezeko la joto.

Ripoti Maalum ya Athari za Ongezeko la Joto kutoka jopo la Kisayansi la Umoja wa Mataifa la Kukabiliana na Mabadiliko ya Athari ya Hali ya Hewa (IPCC), inasema kuwa k joto limeongezeka kufikia 1.5°C na kama jitihada za haraka zakukabiliana nazo hazitofanyika linaweza kufikia 2°C.

Walistushwa pia na kutoonekana kwa baadhi ya wanyama na ndege waliozea kuwaona kwenye hifadhi hiyo.

“Kuna wanyama kama nyani ambao wanapenda kuwapo eneo lenye miti iliyokaribiana, yale maeneo ambao miti imekatwa kwa wingi wanyama hawa wamehama, kwa hivyo  tusipofanya juhudi za kurudisha uoto asili katika hifadhi hii kuna hatari wanyama hawa wanaweza kutoweka kabisa”, aliongeza.

Anarejelea kuwa  wakati wavuna mbao wao wamezama kwenye utengezaji samani na wanawake kukata kuni kwa ajili ya kupikia, binadamu  wengine wanasababisha mlima kuungua moto, ni wakala na watendaji wa hujuma za kijangili na wale wanaorina asali kwa siri ndani ya eneo la hifadhi lililopigwa marufuku ya shughuli za binadamu.

Mara hii akitumia lugha ya bashasha, tofauti na hisia zilizofungua mjadala na Nipashe, anasema wamefanikiwa kupunguza majanga ya moto yaliyokuwa yakitokea kila mara na sasa huchukua hata miaka 2 bila ya moto kitokea.

WALIVYOJIDHATITI

Mwanamazingira Kikoti,  katika wajibu wa mamlaka ya hifadhi Kilimanjaro kwa kushirikiana na wadau wamazingira, wapo katika kipindi endelevu cha   kuzuia barafu kuendelea kuyeyuka mlimani na athari za mabadiliko ya tabia nchi.

 Nipashe inahamisha udadisi wake na kukinga sikio kupata ufafanuzi wa Theonest Kagwebe, Askari Mhifadhi  Namba Moja anayesimamia Idara ya Ujirani Mwema ya KINAPA.

Kagwebe anasimulia aina ya urafiki na vijiji jirani unaofanywa na Mamlaka ya Hifadhi Mikumi kwa vijiji kama Kidogobasi kilichopo wilayani Kilosa, nao KINAPA wamejisogeza kwa jumla ya vijiji 92 vinavyouzunguka Mlima Kilimanjaro, ajenda yao kuu ikiwa ni elimu ya kina kuhusu mazingira na manufaa yanayohusiana nayo.

“Huwa tunazungukia shule zote zilizopo eneo linalozunguka hifadhi na kutoa elimu juu ya umuhimu wa kutunza mazingira katika hifadhi hii. “Pia, tunafanya mikutano kwa kushirikiana na viongozi wa vijiji ili kutoa elimu kwa wanajiji.

“Kuna baadhi ya makosa tukiyakamata huwa hatumpeleki mtuhumiwa polisi bali tunampa elimu. Kwa mfano, ukimkuta mama kakata mti mdogo kwa ajili ya kupikia, kama ni kosa la kwanza huwa tunamuelimisha, akirudia ndio tutampeleka kituo cha polisi,” anasimulia Askari Kagwebe

Kudumisha utamaduni

Kagwebe, akiwa katika ukomavu wake wa askari jamii , anataja staili nyingine ya kufanya kazi yao kudhibiti hujuma hizo za kimazingira, pia uhamasishaji wa jamii hizo kudumisha utamaduni wa kabila lao, ambalo kwa sehemu kubwa ni jamii ya wachagga.

Anaeleza: “Kupitia Idara ya Ujirani Mwema, tunatoa mbegu za mimea ya asili kama vile parachichi, kahawa na ndizi na kuhamasisha wanakijiji wapande kuzunguka nyumba zao, ikiwa ni utamaduni wao, pia kuongeza uoto asili”.

Kiongozi huyo wa askari, anataja eneo lingine wanalowekeza ni urafiki na majirani hao kwa kusaidia miradi mbalimbali inayoombwa na wananchi, lengo ni kuwaonyesha faida inayopatikana kutokana hifadhi hiyo.

 “Mpaka sasa miradi mikubwa ambayo tumeishaikamilisha ni ujenzi wa bwalo lakulia chakula katika Shule ya Sekondari Korikie, iliyoko Kitongoji cha Mamba, Ujenzi wa madarasa katika Shule ya Sekondari ya Zakayo Mosha na ujenzi wa Zahanati ya Kitowo ambazo tumeshazikabidhi kwa Serikali” anasema.

Doria masaa 24

Ofisa Uhifadhi Mwandamizi anayesimamia idara ya Ulinzi na Uoakoaji, Mapinduzi Ndesa  anasimulia kuwa wameona mafanikio kwa miaka 10 sasa, kwakuwa timu ya askari wa hifadhi hiyo wanafanya kazi usiku na mchana kwa kushirikiana na wanavijiji kuhakikisha  wanakomesha ujangili unaoendelea.

 “Kwa mwezi huwa tunakamata majangili wasiozidi 10, kutegemeana na msimu, mfano mwezi wa tatu tumekamata watu 10, kati ya hao 8 walikuwa  wanawake waliokata kuni kwa ajili ya kupikia, hao wawili walikuwa wanakata magogo na umewapeleka kwenye vyombo vya sheria”, anasema

Kauli hio inathibithishwa na Mwenyekiti wa Kijiji cha Msiri, Kata ya Marangu Mashariki, John Mtui, akitoa ushuhuda wa kijiji chake kushirikiana na KINAPA kudhibiti ujangili wa kibiashara.

“Mfano mwezi Aprili, mwaka huu tumekamata wanakijiji wa hapa kwetu wakiwa na kuni mbichi wakitokea msituni, tukawaripoti kwa mhifadhi kwa bahati mbaya wametoroka ila tunawasaka na tukiwapata tutawakabidhi kwa wahifadhi wa KINAPA,” anasema mwenyekiti huyo.

Askari Ndesa anataja mbinu nyingine wanayoitumia kudhibiti uhalifu huo kuwa ni kunafanywa tahmini katika hifadhi hiyo kila, baada ya miezi mitatu kukagua kama kuna ukatwaji wa miti na inapogundulika kuwa kuna dalili ya kukatwa miti eneo fulani hapo kunafanyika doria kali.

 

 Je, wadau wengine wa vita vya kuitetea KINAPA na ustawi wake wana nafasi gani? Usikose makala inayofuata.

Habari Kubwa