Haji Manara na wenzake waburuzwa mahakamani

07Aug 2019
Na Waandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Haji Manara na wenzake waburuzwa mahakamani

MSEMAJI wa Klabu ya Simba ya jijini Dar es Salaam Haji Manara na wenzake watatu wameburuzwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, akidaiwa deni na fidia ya Sh. milioni 83.3 baada ya kupokea bidhaa zenye nembo ya Dela Boss Perfume bila kuzilipia.

MSEMAJI wa Klabu ya Simba ya jijini Dar es Salaam Haji Manara.

Mbali na fedha hizo, mlalamikaji Abu Masoud Al Jahdhamy LLC, ameiomba mahakama kuwaamuru walalamikiwa, Manara, Beatrice Ndungu na Palm General Supply, kumlipa fidia nyingine itayoona zinafaa na gharama za mawakili.

Kesi hiyo ya madai namba 128/2019 ilitajwa jana mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Wanjah Hamza na imepigwa kalenda mpaka Agosti 29, mwaka huu itakapotajwa tena.

Katika madai ya msingi, mlalamikaji amefungua kesi hiyo akiwadai walalamikiwa fedha hizo baada ya kuwasambazia bidhaa yenye nembo ya Dela Boss Perfume 'Tanzania' zilizotengezwa Dubai.

Ilidaiwa kuwa mlalamikaji aliingia mkataba na Manara Desemba 19, 2018 kwa kuchapa bidhaa zenye maneno hayo.

Katika mkataba huo, mlalamikaji alitakiwa kupata asilimia 70 na Manara asilimia 30 na kwamba faida itakayopatikana angemrudishia mlalamikaji gharama za uwekezaji wa kufikisha bidhaa jijini Dar es Salaam.

Januari 21, 2019 mlalamikaji kupitia kampuni ya AMA Trading LLC, ilituma bidhaa hizo jijini Dar es Salaam ambazo zina thamani ya Sh. milioni 46 na zilipokelewa na mlalamikiwa wa pili, Ndungu na wa tatu kama mawakala.

Januari 21, 2019 mlalamikaji alituma fomu ya madai ya Sh. 83,300,000 kwa mlalamikiwa wa pili na wa tatu akitaka kulipwa faida ya uwekezaji na kiasi kilichotumika kununulia bidhaa hizo pamoja na faida.

Walalamikiwa walipokea bidhaa hizo na mpaka sasa hawajalipa chochote pamoja na kudaiwa kwa maneno na maandishi kutoka kwa mlalamikaji.

Mlalamikaji anadai kuwa kutokana na kitendo hicho kimemsababishia usumbufu mkubwa na hasara katika biashara zake.

Habari Kubwa