Hakimu amgomea Nondo  kujitoa

17May 2018
George Tarimo
IRINGA
Nipashe
Hakimu amgomea Nondo  kujitoa

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Wilaya ya  Iringa imetupilia mbali maombi yaliyowasilishwa na Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP), Abdul Omary Nondo,  la kutaka hakimu anayesikiliza kesi yake,  ajitoe kutokana na upande wa utetezi kutokuwa na imani naye.

Wanafunzi Tanzania (TSNP), Abdul Omary Nondo.

Nondo kupitia mawakili wake Jumatano aliwasilisha maombi mahakamani ya kumtaka hakimu huyo, John Mpitanjia, ajitoe kwa madai ya kutokuwa na imani naye kama atamtendea haki.

Katika barua yake ya Nondo alieleza sababu kadhaa za kumtaka Hakimu Mpitanjia  kujiondoa.

Alidai kukosa imani kwa Mpitanjia kutokana na  hakimu huyo kukutana na mmoja wa mashahidi ambaye ni shahidi wa tatu kutoka upande wa Jamhuri, Paulo Emanuel Kisabo, ambaye ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na pia ni mkurugenzi wa idara ya sheria na kumuhoji kama anaendelea kuwasiliana na mshtakiwa ambaye ni Nondo.

Sababu ya pili, Nondo anadai kila kesi hiyo inapoletwa mahakamani  Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Iringa, Deusdedit Kasindo, amekuwa akionekana na hakimu Mpitanjia kabla na baada ya kesi hiyo.

Sababu ya tatu ya Nondo kumkataa Hakimu Mpitanjia ni mahusiano na mawasiliano mazuri na upande wa Jamhuri huku akionyesha  mahusiano mabaya na upande wa mshtakiwa.

Nondo alidai ofisi za makamanda wa polisi wa mikoa ya Iringa na Dar es Salaam walitoa taarifa kwenye vyombo vya habari kuwa alijiteka na hakutekwa na watu wasiojulikana.

Sababu hizo ziliwasilishwa mahakamani na wakili wa utetezi ambaye ni wakili kiongozi, Jebra Kambole,  akisaidiwa na Chance Luwoga.

Jana Hakimu Mpitanjia aligoma kujiondoa kwenye shauri hilo na kusema malalamiko yaliyotolewa hayana ushahidi wa kutosha, hivyo kujitoa ni sawa na kuisumbua mahakama kwa vile italazimika kumpanga hakimu mwingine.

Kesi hiyo ilianza kusikilizwa majira ya saa 6:00 mchana na ilipofika saa 6:37 ilihairishwa hadi kesho kwa kusikiliza mashahidi wawili ambao walitoa ushahidi na hawakumalizia kutokana na mabishano ya sheria kwa pande mbili  za Jamhuri na utetezi.

Akisoma maamuzi ya mahakama,  Hakimu Mkazi Mpitanjia, alisema anaheshimu mawasilisho yaliyowasilishwa na mawakili wa pande zote mbili katika malalamiko yaliyowasilishwa na Nondo kwenye barua yake ya Mei 13 , mwaka 2018.

Mpitianjia alisema amezingatia heshima na nguvu iliyopewa mahakamani katika katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ibara ya 107 (a) sehemu ya kwanza na ya pili kifungu kidogo inayosema mahakama ndicho chombo cha mwisho cha kutoa haki.

Akinukuu vifungu hivyo, alisema mahakama ndicho chombo cha mwisho cha utoaji haki Tanzania na katika kutenda haki, mahakama itazingatia misingi ya usawa, bila kujali nafasi yake mtu ya kiuchumi katika jamii, kutochelewesha haki bila sababu za msingi na kutenda haki bila kufungwa na mambo ya kiufundi au ya kisheria.

Hivyo kwa kuzingatia jukumu hilo la mahakama kama mhimili unaojitegemea bila kuingilia na mtu ama chombo chochote, haoni sababu za yeye kujiondoa katika kusikiliza shauri hilo.

Baada ya kutoa maamuzi ya mahakama, upande wa Jamhuri ukiwakilishwa na Alex Mwita uliomba kupangiwa tarehe nyingine, ombi ambalo upande wa utetezi uliowakilishwa na wakili Jebra Kambole na mwenzake, Chance Luwoga waliomba shauri hilo litajwe kesho.

Nondo anatuhumiwa kutenda makosa mawili ambayo ni kusambaza taarifa za uongo akiwa Ubungo jijiji Dar es Salaam na kosa la pili ni kutoa taarifa za uongo kwa mtumishi wa umma ambaye ni askari polisi wa Kituo cha Mafinga wilayani Mufindi Mkoa wa Iringa.

Habari Kubwa