Hakimu atoa somo taratibu kukiri kosa kwa DPP

24Nov 2020
Hellen Mwango
Dar es Salaam
Nipashe
Hakimu atoa somo taratibu kukiri kosa kwa DPP

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imesema jukumu la washtakiwa wenye nia ya kukiri makosa na kumaliza kesi kwa njia ya majadiliano na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP) ni kufuata utaratibu sahihi badala ya kutaka majibu ya maombi yao mahakamani.

Hakimu Mkazi Mkuu, Kassian Matembele, alisema jana wakati kesi ya kutakatisha Sh. bilioni 1.477 inayomkabili Mkurugenzi wa zamani wa Mipango, Ufuatiliaji na Tathmini wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Kulthum Mansoor, ilipopangwa kutajwa.
Kesi hiyo ilitajwa jana kwa njia ya mahakama mtandao.

Hakimu Matembele alisema utaratibu wa kumaliza kesi kwa njia ya majadiliano ni kati ya mshtakiwa au ndugu na Ofisi ya DPP hivyo inawapaswa kufuata utaratibu sahihi wa kufuatili katika ofisi ya DPP mpaka wanapopata majibu badala ya kwenda kuuliza majibu mahakamani.

“Siyo kazi ya mahakama kufuatilia hilo, mahakama inahusika tu pale ambapo mmeshafikia makubaliano ndipo inahusika katika utekelezaji wa makubaliano," alisema.

Awali, Wakili wa Serikali, Wankyo Simon, alidai shauri hilo lilikwenda mahakamani hapo kwa ajili ya kutajwa, lakini upelelezi bado na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa.

Baada ya kutoa hoja hiyo upande wa utetezi katika kesi hiyo uliomba upande wa mashtaka kuharakisha upelelezi huku akieleza maombi ya kumaliza kesi kwa njia ya majadiliano na DPP ilipofikia.

Kupitia Wakili wa Utetezi, Elia Mwingira, alisema haoni ushirikiano wala maendeleo yoyote katika suala la kumaliza kesi kwa njia ya majadiliano huku akisema kuwa ofisi ya DPP iliwaambia watapata majibu kutoka kwa ofisi ya mawakili, lakini mpaka sasa hajapata majibu kamili.

Akijibu hoja hiyo, Wankyo alidai kuwa upande wa utetezi unaendelee kufuatilia na kuwataka wasikate tamaa pamoja na kuwa upelelezi haujakamilika watajitahidi kuharakisha.

Katika kesi ya msingi Kulthum anakabiliwa na mashtaka manane likiwamo la kughushi, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kutakatisha fedha kiashi cha Sh. 1,477,243,000.

Habari Kubwa