Hakimu kikwazo marais wa Simba

26Apr 2018
Hellen Mwango
Nipashe
Hakimu kikwazo marais wa Simba

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, imepiga kalenda kusikiliza maelezo ya awali ya kesi ya kughushi na kutakatisha Dola za Marekani 300,000 inayowakabili Rais wa Klabu ya Simba, Evance Aveva na Makamu wake, Godfrey Nyange a.k.a Kaburu hadi wiki ijayo kutokana na udhuru wa hakimu.

Makamu wa rais wa klabu ya Simba, Godfrey Nyange maarufu kama Kaburu, akitolewa mahabusu kupelekwa mahakamani kusikiliza kesi inayomkabili, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam jana. PICHA: HALIMA KAMBI

Kesi hiyo ilitajwa jana mbele ya Hakimu Mkazi, Martha Mpanze, baada ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, aliyepangiwa kusikiliza kesi hiyo kuwa na udhuru wa kikazi.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Leonard Swai, alidai kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya kuwasomea washtakiwa maelezo ya awali, lakini kwa kuwa hakimu anayeisikiliza hayupo aliomba mahakama kupanga tarehe nyingine.

Hakimu alisema kesi hiyo itasikilizwa maelezo ya awali Aprili 30, mwaka huu.

Aprili 3,mwaka huu upande wa Jamhuri ulidai upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na uliomba kumuunganisha mshtakiwa mwingine kabla ya kusomwa maelezo hayo.

Katika kesi ya msingi, Aveva na Kaburu wanakabiliwa na mashtaka matano ya kughushi, kuwasilisha nyaraka ya uongo na kutakatisha fedha Dola za Marekani 300,000.

Washtakiwa hao inadaiwa walikula njama ya kughushi fomu ya maombi ya kuhamisha fedha ya Machi 15,2016 wakionyesha Klabu ya Simba inalipa mkopo wa Dola za Marekani 300,000 kwa Evans Aveva wakati si kweli.

Habari Kubwa