Hali ya Lissu tete

14Sep 2017
Gwamaka Alipipi
Nipashe
Hali ya Lissu tete

HALI ya Mwanasheria Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu bado ni tete, kwa mujibu wa maofisa wa chama hicho wanaomuuguza jijini Nairobi, Kenya.

HOSPITALI ALIYOLAZWA tUNDU LISSU

Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki na Rais wa Chama cha Wanasheria (TLS), alishambuliwa kwa kupigwa risasi mjini Dodoma na watu wasiojulikana wakati akiwasili nyumbani kwake Area D akitokea bungeni Alhamisi ya wiki iliyopita.

Baada ya tukio hilo, Lissu (49), aliwahishwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma ambako alipatiwa matibabu ya awali kabla ya kusafirishwa kwenda Kenya kwa ajili ya matibabu zaidi.

Akiwa jijini Nairobi jana, Mkuu wa Idara ya Uenezi Chadema, Hemed Ali, aliiambia Nipashe kuwa hali ya kiafya ya mtaalamu huyo wa sheria bado ni tete.

"Hali yake bado ni mbaya, ila maendeleo ya kuwa vizuri yanaelekea kuwa chanya, ila ameumizwa sana," alisema Ali.

Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Vincent Mashinji, aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuwa hali ya Lissu ilibadilika ghafla na kusababisha madaktari kumwekea mashine ya kumsaidia kupumua.

Dk. Mashinji pia alisema risasi alizopigwa Lissu zilisababisha kuvunjika kwa mguu wa kulia, mkono wa kushoto na nyonga.

Habari Kubwa