Halmashauri Tunduru yapata hati safi miaka mitano mfululizo

24May 2020
Gideon Mwakanosya
SONGEA
Nipashe
Halmashauri Tunduru yapata hati safi miaka mitano mfululizo

MKUU wa Mkoa wa Ruvuma, Christina Mndeme, amewapongeza  madiwani,wabunge na watalaam wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru kwa kupata hati safi kwa mujibu wa Ripoti ya CAG ya Hesabu za mwaka wa fedha unaoishia Juni 30,2019.

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme akipongeza Tunduru kupata hati safi mara tano mfululizo.

Mndeme ametoa pongezi hizo wakati anafungua kikao maalum cha Baraza la madiwani cha kujadili taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kuhusu hoja na mapendekezo ya Hesabu za TAMISEMI kwa mwaka wa fedha wa 2018/2019 mjini Tunduru.

“Kitendo cha kupata hati safi ni  matokeo ya utendaji kazi mzuri wenye mshikamano na ushirikiano kati ya watalaam wa Halmashauri na madiwani,hii ni kutokana na Halmashauri kuundwa na pande mbili,inapotekea mnafanya vizuri,hata sisi viongozi katika ngazi ya Mkoa tunafarijika sana hongereni sana’’, amesema Mndeme.

Hii ni mara ya tano mfululizo kwa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru kupata hati safi kuanzia mwaka wa fedha wa 2014/2015 hadi 2018/2019 ambapo Mndeme amesisitiza kuwa kupata hati safi mfululizo iwe chachu ya kufanya vizuri zaidi.

Katika kikao hicho Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma amemwagiza Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma Steven Ndaki kuhakikisha miradi yote ya maendeleo katika Halmashauri zote nane za Mkoa wa Ruvuma inakaguliwa na kufanyiwa tathimini.

Baadhi ya wananchi na watalaam wakifuatilia baraza maalum la Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru.

 “Iwapo kuna uzembe uliosababisha  miradi kutotekelezwa kwa viwango vinavyotakiwa nipate taarifa ya hatua stahiki zilizochukuliwa kwa watumishi wazembe kabla au ifikapo tarehe 30 Septemba,2020’’, amesisitiza Mndeme.

Mndeme pia ameagiza kupata sababu ambazo zimekuwa zinasababisha hoja za aina moja kujitokeza mara kwa mara  na hoja ambazo hazijafungwa ambapo ameagiza kupata orodha ya majina ya watumishi husika na vyeo vyao na hatua walizochukuliwa kabla ya Juni 30 mwaka huu. 

Habari Kubwa