Halmashauri ya mji wa Mbinga wanufaika na bilioni 3.5 za Magufuli

28May 2020
Gideon Mwakanosya
Mbinga
Nipashe
Halmashauri ya mji wa Mbinga wanufaika na bilioni 3.5 za Magufuli

SERIKALI imetoa zaidi ya shilingi bilioni 3.5 kwa Halmashauri ya Mji wa Mbinga mkoani Ruvuma kwa ajili ya ujenzi wa majengo tisa.

Jengo la Halmashauri ya Mji wa Mbinga ambalo limekamilka na
kuanza kutumika,limegharimu sh.bilioni 2.9

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Mbinga Grace Quentin ametoa taarifa ya miradi hiyo kwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme alipokagua miradi hiyo ikiwemo nyumba ya Mkurugenzi iliyogharimu sh.milioni 300,nyumba saba za wakuu wa Idara zimegharimu sh.milioni 350 na jengo la Halmashauri limegharimu sh.bilioni 2.9 ambalo limekamilika na kuanza kutumika.

Akizungumzia mradi wa nyumba za watumishi na nyumba ya Mkurugenzi ambayo itakuwa na ghorofa moja,Quentin amesema mradi  kwa ujumla wake umefikia asilimia 70 na kwamba mradi ulianza kutekelezwa Aprili na unatarajia kukamilika Juni 2020.

“Mradi huu wa nyumba za watumishi utasaidia sana wakuu wa Idara,badala ya Halmashauri kuwalipa pango la nyumba,tutakuwa tumewasaidia nyumba hizi,mradi unafanyika kwa force account na  Msimamizi Mkuu wa mradi ni TARURA’’,amesema Quentin.

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme akitoa maelekezo baada ya kukagua mradi wa nyumba za watumishi Halmashauri wa Mji wa Mbinga.

Akizungumza baada ya kukagua miradi hiyo,Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme kwa niaba ya wananchi wa Mbinga,amemshukuru Rais Dkt John Magufuli kwa kuruhusu kiasi hicho cha mabilioni ya fedha yaliyowezesha kujengwa jengo bora la Halmashauri ya Mji wa Mbinga.

“Tuna kila sababu ya kumshukuru Rais wetu kwa zawadi hii kubwa,kwa niaba ya serikali nawapongeza  wana Mbinga Mji kwa kupata jengo hili zuri na rafiki la kutolea huduma’’,alisisitiza.

Amesema kiasi hicho cha fedha kimejenga majengo tisa,moja la Halmashauri likiwa limekamilika na majengo mengine nane yakifikia asilimia 70 ya ujenzi ambapo amesisitiza kuwa kazi ni nzuri  ambapo ameahidi kuzipeleka Halmashauri nyingine kwenda kujifunza katika Halmashauri hiyo.

Mradi wa nyumba saba za watumishi katika Halmashauri ya Mji wa Mbinga,ujenzi umefikia asilimia 66.

Hata hivyo amesema katika Mkoa wa Ruvuma anasimamia ujenzi wa majengo matatu ya Halmashauri yakiwemo Halmashauri ya Nyasa,Madaba na jengo la Mbinga Mji ambalo licha ya ujenzi wake kuanza nyuma limekamilika kabla ya waliotangulia kuanza ujenzi.

Amesisitiza kuwa Halmashauri ya Mji wa Mbinga wamekuwa mfano katika Mkoa kwa kukamilisha kazi na kuzishinda Halmashauri nyingine zilizopata fedha mapema na kuanza kazi mapema ambapo hadi sasa ujenzi wao haujakamilika hadi ameamua kuwapelekwa TAKUKURU kuchunguza.

Amemwagiza Mkurugenzi kuhakikisha kuwa jengo nzuri liwahudumia wananchi vizuri na kutoa maamuzi mema kwa manufaa ya wananchi wa Mji wa Mbinga na Tanzania.

Habari Kubwa