Halmashauri yanunua gari la milioni 80 kusimamia miradi

29Nov 2021
Elizabeth John
NJOMBE
Nipashe
Halmashauri yanunua gari la milioni 80 kusimamia miradi

Halmashauri ya Wilaya ya Njombe kupitia mapato yake ya ndani imenunua gari moja aina ya Ford Ranger yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 80 ambayo itaenda kutumika katika idara ya ujenzi ndani ya halmashauri hiyo kwenda kurahisisha shughuli za miradi.

Akizungumza na wananchi waliofika katika viwanja vya stendi ya zamani mjini Njombe wakati wa uzinduzi wa maadhimisho ya Sherehe za Uhuru kimkoa, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Njombe,Sharifa Nabalang'anya amesema kuwa licha ya upungufu wa magari katika idara nyingine ndani ya halmashauri hiyo wameamua kununua gari hiyo kupitia mapato yake ya ndani.

Mkuu wa Mkoa wa Njombe Injinia Marwa Rubirya ndiye aliyefanya uzinduzi na kukabidhi gari hilo kwa halmashauri hiyo ambapo ameelekeza gari hilo ni lazima likatumike kwa kazi iliyokusudiwa ili kuweza kuleta tija.

Uzinduzi wa maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru kimkoa umefanyika katika viwanja vya stendi ya zamani huku wajasiriamali mbalimbali wakitumia kusanyiko hilo kama fursa na  kupeleka bidhaa mbalimbali.

Habari Kubwa