Hamad Rashid ajinadi kwa kero za Muungano

10Jul 2020
Rahma Suleiman
Zanzibar
Nipashe
Hamad Rashid ajinadi kwa kero za Muungano

MWENYEKITI wa ADC, Hamad Rashid Mohamed, amechukua fomu ya kuomba kuwania urais wa Zanzibar kupitia chama hicho ikiwa ni mara ya pili kugombea nafasi hiyo.

Mwaka 2015, aligombea nafasi hiyo lakini kura alizopata hazikumpatia ushindi.

Akizungumza na waandishi wa habari jana baada ya kuchukua fomu hiyo, Hamad alisema miongoni mwa mambo atakayohakikisha anayapatia ufumbuzi akipata ridhaa ya kuwa urais, ni kutatua kero za Muungano.

Hamad ambaye ni Waziri wa Afya wa Zanzibar, alisema kuna baadhi ya kero za Muungano ambazo Wazanzibari kwa muda mrefu wamekuwa wakilalamikia, lakini baadhi hadi leo bado hazijapata ufumbuzi, hivyo ni imani yake kwamba akipata ridhaa zitaondoka.

Alisema vipaumbele vyake vingine ni kujadiliana na serikali ya Muungano kutoa urais wa nchi mbili kwa wale wenye kutaka hivyo, akidai kuwa lengo ni kuona maendeleo ya nchi yanapatikana.

Kuhusu elimu, alisema miongoni mwa mambo atakayosimamia ni kulipia mwaka wa mwanzo wa masomo kwa wanafunzi wote hata waliokosa mikopo, kutenganisha wanaume na wanawake katika shule yaani wanaume wawe na madarasa yao na wanawake vivyo hivyo.

Alisema hivi sasa wanafunzi wengi wa Zanzibar shule wanazosomea mazingira yake hayako salama katika majengo, hivyo atakapopata ridhaa ya kuongoza Zanzibar itakuwa na shule za ghorofa.

Licha ya serikali ya Zanzibar kuweka suala la elimu bure kwa ngazi ya msingi mpaka ualimu, chama chake kimeandaa utaratibu wa kuweka hadi shahada ya kwanza kuwa bure kwa wanafunzi wote.

Habari Kubwa