Hanang’ kinara mwitikio upataji chanjo corona

20Oct 2021
Jaliwason Jasson
Babati
Nipashe
Hanang’ kinara mwitikio upataji chanjo corona

WILAYA ya Hanang’, mkoani Manyara, inatajwa kuwa kinara wa mwitikio chanya wa wananchi kujitokeza kupata chanjo ya UVIKO-19, baada ya kutumika kikamilifu kwa dozi 2,050 ya chanjo ya Johnson & Johnson.

Kwa mujibu wa takwimu za kampeni hiyo, iliyosomwa jana na Mkuu wa wilaya hiyo, Janeth Mayanja, mwitikio huo unatoa picha kwamba elimu, dhidi ya chanjo hiyo imewafikia wananchi ingawa bado juhudi za makusudi zinahitajika vijijini.
Mayanja aliyasema hayo jana, wakati akielezea mafanikio ya wananchi wa eneo hilo juu ya uchanjaji wa chanjo ya UVIKO-19.

“Agosti mwaka huu, tulipokea dozi ya chanjo 1,000 aina ya Janssen (Johnson & Johnson) na kuanza kuitoa kwa wahitaji. Lakini Septemba 21 mwaka huu, tukaongezewa tena dozi nyingine 1,000 za aina hiyo hiyo ya Janssen,” alisema Mayanja na kuongeza:

“Oktoba 11 tuliongezewa tena dozi nyingine 50 za chanjo ya UVIKO-19 za aina hiyo hiyo ya Janssen, nazo zimekwisha hivyo kufikisha jumla ya chanjo zote kuwa 2,050.”

Aidha, mkuu huyo wa wilaya, kampeni hiyo ilizindua wilayani humo Agosti 5 mwaka huu. Awali chanjo ilikuwa inatolewa kwenye vituo vitatu pekee, lakini baadaye vituo viliongezwa hadi kufikia 25.

Alisema chanjo hizo zilisambazwa kwenye vituo 25 vya kutolea huduma ambavyo ni Gitting, Barjomot, Gendabi, Dawar, Bassotu, Getanuwas, Murjanda, Tumaini na Endasak.

Alitaja vituo vingine ni Katesh, Simbay, Waama, Waranga, Balangdalalu, Murumba, Nangwa, Dirma, Dumbeta, Gidahababieg, Sirop, Masakta, Bassodesh, Mulbadaw, Setchet na Gidagamowd.

“Uhamasishaji umefanyika katika taasisi za umma na binafsi na maeneo yenye mikusanyiko chanjo zilizotolewa ni 2045 na kubakiwa na chanjo tano, ambazo zitamalizika wakati wowote, hata hivyo tumeomba chanjo zaidi,” alisema.

Alisema uhamasishaji unaendelea na aliwashukuru viongozi wa dini, wazee maarufu, wadau,wakuu wa taasisi na wananchi wote kwa kufanikisha suala hilo.

Mkazi wa Kijiji cha Endasak, Erasto Elia alisema elimu iliyotolewa na wataalam wa afya imechangia wao kushiriki kikamilifu shughuli ya kupatiwa chanjo ya UVIKO-19.

Alisema awali baadhi ya watu walizusha maneno ya kupotosha na kuwapa watu hofu kuwa chanjo hiyo ina matatizo kwa wananchi jambo ambalo siyo kweli.

Habari Kubwa