Hans Poppe akiri kununua nyasi Simba

20Oct 2018
Hellen Mwango
Dar es Salaam
Nipashe
Hans Poppe akiri kununua nyasi Simba

MFANYABIASHARA Zacharia Hans Poppe, amekiri mahakamani anuani yake na kwamba ni kweli alifanya mchakato wa ununuzi nyasi bandia.

MFANYABIASHARA Zacharia Hans Poppe picha na mtandao

Hans Poppe na vigogo wengine wawili wa klabu ya Simba, akiwamo Rais na Makamu wa Klabu ya Simba,  Evans Aveva na Godfrey Nyange, maarufu kama Kaburu, wanakabiliwa na  mashtaka tisa, ikiwamo matumizi mabaya ya ofisi, kughushi, kuwasilisha nyaraka za uongo na kutakatisha Dola za Marekani 300,000.

Washtakiwa hao walisomewa maelezo ya awali mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Thomas Simba.

Upande wa Jamhuri uliongozwa na Mawakili wa Serikali Waandamizi, Shadrack Kimaro na Mutalemwa Kishenyi wakati ule wa utetezi uliongozwa na mawakili Nehemia Nkoko, Nestory Wandiba na Augustine Shio.

Kimaro alidai kuwa katika hati ya mashtaka wanasomeka washtakiwa wanne.

Alidai kuwa mshtakiwa wa nne, Franklin Lauwo aliahidi kujisalimisha Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru)  lakini mpaka jana asubuhi  alikuwa hajajisalimisha.

"Mheshimiwa chini ya kifungu cha 91 kidogo cha (1) cha Mwenendo wa Sheria ya Makosa ya Jinai (CPA),  upande wa Jamhuri tunaomba kuondoa shtaka linalomhusu mshtakiwa huyo ili kesi iendelee kusikilizwa maelezo ya awali, "alidai Kimaro.

Upande wa utetezi ulikubaliana na ombi la Jamhuri na Hakimu alisema shtaka hilo linaondolewa kwa sasa kwa sababu mshtakiwa hayupo.

Akiwasomea maelezo ya awali,  Kimaro alidai kuwa Aveva alikuwa Rais wa Klabu ya Simba,  Kaburu Makamu wa Rais na Hans Poppe ni mfanyabiashara.

Alidai kuwa Machi 12, 2016 klabu ya Simba ililipwa Dola za Marekani 319,212 kutoka klabu ya Etoile Sportive Du Sahel ya Tunisia ikiwa ada ya kumhamisha Emmanuel Okwi kwenda Tunisia.

Ilidaiwa kuwa fedha hizo zilihamishiwa katika akaunti ya klabu ya Simba iliyoko benki ya CRDB tawi la Azikiwe ambayo mshtakiwa wa kwanza na wa pili ni watia saini.

Kimaro alidai kuwa Machi 15, 2016 zilihamishwa Dola 300,000 kutoka akaunti ya klabu ambayo rais na makamu wake ndio watia saini kwenda akaunti binafsi ya Aveva iliyoko benki ya Barclays, tawi la Ohio ambayo mshtakiwa huyo ni mtia saini pekee.

"Uhamisho wa fedha hizo zinazodaiwa zilikopwa na klabu ya Simba haukuwa na baraka na Kamati ya Uendaji ya klabu hiyo," alidai Kimaro wakati akiwasomea washtakiwa maelezo hayo.

Ilidaiwa kuwa fedha hizo zilianza kuhamishwa kidogo kidogo.

Aveva alidaiwa kuhamisha Dola 62,183 kwenda akaunti ya kampuni ya Ninah Guangzhou Trading Limited kama malipo ya kununua nyasi bandia kwa ajili ya ujenzi wa kiwanja wa klabu hiyo ulioko Bunju, Kinondoni, jijini Dar es Salaam.

Ilidaiwa kuwa mshtakiwa alihamisha Dola 50,000 kwenda kwa Lauwo kama malipo ya ujenzi wa kiwanja cha klabu,  wakati kampuni yake Ranky Infrastructure & Engineering Limited haijasajiliwa na Bodi ya Usajili wa Makandalasi (CRB).

Ilidaiwa kuwa washtakiwa wote watatu walitengeneza hati ya malipo ya uongo na kuipeleka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)  wakionyesha kuwa nyasi bandia zilinunuliwa kwa Dola 40,000 kwa nia ya kukwepa kodi ndipo walikamatwa na kushtakiwa.

Aveva alikubali anuani yake na wadhifa wale kwenye klabu,  Kaburu alikubali anuani yake na wadhifa wake pia huku Hans Poppe alikiri anuani yake.

"Ni kweli mimi mfanyabiashara, nakubali nilifanya mchakato wa kununua nyasi bandia," alidai Hans Poppe baada ya kusomewa maelezo ya awali.

Hakimu Simba alisema baada ya washtakiwa kukana tuhuma dhidi yao kesi hiyo itaanza kusikiliza ushahidi wa Jamhuri Oktoba 31, mwaka huu.

Katika kesi ya msingi,  Kimaro alidai kuwa katika tarehe tofauti kati ya Machi 10 na 16, 2016 Aveva na Kaburu walikula njama ya kutenda kosa la matumizi mabaya ya ofisi.

Shtaka la pili,  ilidaiwa kuwa katika tarehe tofauti kati ya Machi 10 na 16, 2016 jijini Dar es Salaam, Aveva na Kaburu walifanya matumizi mabaya ya madaraka kwa kuandaa hati ya kuhamisha Dola za Marekani 300,000 kutoka akaunti ya Klabu ya Simba benki ya CRDB tawi la Azikiwe kwenda akaunti binafsi ya Aveva iliyoko benki ya Barclays tawi la Uhio.

Upande huo wa Jamhuri ulidai kuwa shtaka la tatu, Machi 15, 2016 Aveva na Kaburu, wote kwa pamoja walighushi fomu ya kuhamisha fedha ya tarehe hiyo wakionyesha kwamba Klabu ya Simba inalipa deni la Dola za Marekani 300,000 kwa Rais wake, Aveva.

Katika shtaka la nne, ilidaiwa kuwa Machi 15, mwaka 2016 katika benki ya CRDB tawi la Azikiwe, Aveva aliwasilisha fomu ya kuhamisha fedha zilizoghushiwa ya terehe hiyo akinyesha kwamba Klabu ya Simba imeomba kuhamisha Dola za Marekani 300,000 huku akijua si kweli.

Katika shtaka la tano, ilidaiwa kuwa kati ya Machi 10, 2016 jijini Dar es Salaam,  
Aveva alijilipa na kutakatisha Dola za Marekani 187,817 kutoka benki ya Barclays tawi la Uhio, huku akijua zimetokana na kughushi.

Kimaro alidai katika shtaka la sita, kati ya Machi 10 na 16, 2016  Kaburu alitakatisha fedha baada mshtakiwa huyo wa pili kumsaidia Aveva kupata Dola za Marekani 187,817.

Katika shtaka la saba, kati ya Machi 10 na Mei 30, 2016, jijini Dar es Salaam, Aveva, Kaburu na Hans Poppe walighushi hati  ya malipo wakidai wamenunua nyasi bandia  zenye thamani ya Dola za Marekani 40,577 huku wakijua si kweli.

Ilidaiwa katika shtaka la nane kuwa,  kati ya Machi 10 na Mei 30, 2016 kwa makusudi alionyesha nyaraka za kughushi kwa  Levison Kasulwa akionyesha kuwa klabu hiyo imenunua nyasi bandia  kutoka Kampuni ya Nina Guangzhou Trading Limited huku akijua si kweli.

Ilidaiwa katika shtaka la tisa,  kati ya Machi 10 na Septemba 30, 2016 jijini Dar es Salaam,  Aveva, Kaburu na Pope,  walitoa maelezo ya uongo na kuwasilisha nyaraka za kughushi wakionyesha kuwa Klabu ya Simba imenunua nyasi bandia kutoka Kampuni ya Nina Guangzhou Trading Limited zenye thamani ya Dola za Marekani 40,577 huku wakijua si kweli.

Washtakiwa walikana mashtaka yao.

Poppe yuko nje kwa dhamana na Aveva na Kaburu wako mahabusu kutokana na mashtaka ya kutakatisha fedha kutokuwa na dhamana.

Habari Kubwa