Hans Poppe aunganishwa kesi ya vigogo wa Simba

17Oct 2018
Hellen Mwango
DAR ES SALAAM
Nipashe
Hans Poppe aunganishwa kesi ya vigogo wa Simba

HATIMAYE Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe, ameunganishwa katika kesi inayowakabili Rais wa Simba, Evans Aveva na makamu wake Godfrey Nyange, maarufu kama Kaburu.

Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya klabu ya Simba, Zakaria Hanspoppe (wa pili kushoto), akiwa katika chumba cha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam jana, kabla ya kusomewa mashtaka akiunganishwa na Rais wa klabu hiyo, Evans Aveva (wa pili kulia) na Makamu wake, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ (katikati), katika kesi ya kughushi na utakatishaji fedha inayoendelea mahakamani hapo. PICHA: MIRAJI MSALA

Vigogo hao wa Simba wanakabiliwa na mashtaka tisa, yakiwamo matumizi mabaya ya ofisi, kughushi, kuwasilisha nyaraka za uongo na kutakatisha Dola za Marekani 300,000.

Ilidaiwa kuwa washtakiwa walitakatisha dola hizo baada ya kudanganya kuwa Klabu ya Simba imenunua nyasi bandia kutoka Kampuni ya Nina Guangzhou Trading Limited.

Poppe aliunganishwa na wenzake jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Thomas Simba, aliyepangiwa kusikiliza kesi hiyo.

Upande wa Jamhuri uliongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Shadrack Kimaro na Wakili wa Serikali Imani Mtume wakati ule wa utetezi ukiongozwa na Mawakili Nestory Wandiba, Augustine Shio na Benedict Ishabakaki.

Kimaro alidai mahakama iliagiza kumtafuta Poppe ili aunganishwe katika kesi hiyo.

"Mheshimiwa Hakimu kutokana na amri ya kumtafuta Hans Poppe, Mungu amejalia amejitokeza tunaomba kumuunganisha katika kesi hii," alidai Kimaro.

Hakimu alisema mahakama yake imeridhia mshtakiwa huyo kuunganishwa na wenzake.

Akiwasomea hati mpya ya mashtaka, Kimaro alidai kuwa katika tarehe tofauti kati ya Machi 10 na 16, 2016 Aveva na Kaburu walikula njama ya kutenda kosa la matumizi mabaya ya ofisi.

Shtaka la pili, ilidaiwa kuwa katika tarehe tofauti kati ya Machi 10 na 16, 2016 jijini Dar es Salaam, Aveva na Kaburu walifanya matumizi mabaya ya madaraka kwa kuandaa hati ya kuhamisha Dola za Marekani 300,000 kutoka akaunti ya Klabu ya Simba benki ya CRDB tawi la Azikiwe kwenda akaunti binafsi ya Aveva iliyoko benki ya Barclays tawi la Ohio.

Upande huo wa Jamhuri ulidai kuwa shtaka la tatu, Machi 15, mwaka 2016 Aveva na Kaburu, wote kwa pamoja walighushi fomu ya kuhamisha fedha ya tarehe hiyo wakionyesha kwamba Klabu ya Simba inalipa deni la Dola za Marekani 300,000 kwa Rais wake Aveva.

Katika shtaka la nne, ilidaiwa kuwa Machi 15, 2016 katika benki ya CRDB tawi la Azikiwe lililoko Ilala, Dar es Salaam, Aveva aliwasilisha fomu ya kuhamisha fedha zilizoghushiwa ya terehe hiyo akinyesha kwamba Klabu ya Simba imeomba kuhamisha Dola za Marekani 300,000 huku akijua si kweli.

Katika shtaka la tano, ilidaiwa kuwa kati ya Machi 10, 2016 jijini Dar es Salaam, Aveva alijilipa na kutakatisha Dola za Marekani 187,817 kutoka benki ya Barclays tawi la Ohio, huku akijua zimetokana na kughushi.

Swai alidai shtaka la sita, kati ya Machi 10 na 16, 2016 Kaburu alitakatisha fedha baada mshtakiwa huyo wa pili kumsaidia Aveva kupata Dola za Marekani 187,817.

Katika shtaka la saba, kati ya Machi 10 na Mei 30, 2016, jijini Dar es Salaam, Aveva, Kaburu na Poppe walighushi hati ya malipo wakidai wamenunua nyasi bandia zenye thamani ya Dola za Marekani 40,577 huku wakijua si kweli.

Ilidaiwa katika shtaka la nane kuwa, kati ya Machi 10 na Mei 30, 2016 kwa makusudi alionyesha nyaraka za kughushi kwa Levison Kasulwa kuwa klabu hiyo imenunua nyasi bandia kutoka Kampuni ya Nina Guangzhou Trading Limited huku akijua si kweli.

Swai alidai shtaka la tisa, kati ya Machi 10 na Septemba 30, 2016 jijini Dar es Salaam, Aveva, Kaburu na Poppe, walitoa maelezo ya uongo na kuwasilisha nyaraka za kughushi wakionyesha kuwa Klabu ya Simba imenunua nyasi bandia kutoka Kampuni ya Nina Guangzhou Trading Limited zenye thamani ya Dola za Marekani 40,577 huku wakijua si kweli.

Washtakiwa wote walikana mashtaka hayo na upande wa Jamhuri ulidai kuwa hauna pingamizi la dhamana dhidi ya Poppe.

Pia, Jamhuri ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo imekamilika na unaomba tarehe ya kusikiliza maelezo ya awali.

Wakili wa utetezi Shio alidai kuwa mshtakiwa Poppe ni mgonjwa na alikuwa kwenye matibabu nchini Marekani, lakini alipopata taarifa kupitia vyombo vya habari kwamba anatafutwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), alipopata nafuu alimwagiza yeye kama wakili wake kuiandikia barua taasisi hiyo.

"Niliiandikia Takukuru barua kwamba Poppe amepata nafuu, saa 7:25 usiku wa kuamkia Oktoba 15, mwaka huu mshtakiwa aliingia nchini na kujikabidhi mikononi mwa taasisi hiyo hadi jana (juzi) alipoachiwa kwa dhamana na leo (jana) amekuja mahakamani kukabiliana na tuhuma zinazomkabili anapatikana wakati wowote tunaomba dhamana," alidai Wakili Shio.

Hakimu Simba alisema kwa kuwa upande wa Jamhuri hauna pingamizi la dhamana, mahakama inamtaka mshtakiwa kuwa na wadhamini wawili wanaotoka taasisi zinazotambulika watakaosaini hati ya dhamana ya Sh. milioni 15 kila mmoja.

Mshtakiwa Poppe alitimiza masharti hayo na kesi hiyo itasikilizwa maelezo ya awali Oktoba 19, mwaka huu.

Aprili 30, mwaka huu upande wa Jamhuri ulibadilisha hati ya mashtaka kutoka washtakiwa wawili na kuongeza wengine idadi yao ikafikiwa wanne.

Hata hivyo, Jamhuri ulidai kuwa upelelezi umekamilika lakini uliomba hati ya kukamatwa Hans Poppe na mfanyabiashara Franklin Lauwo.

Upande wa utetezi ulipinga uliomba washtakiwa ambao hawajakamatwa waondolewe kwenye hati ya mashtaka ili kesi iendelee kusikilizwa.

Juni 12, mwaka huu mahakama hiyo iliyoketi chini ya Hakimu Simba ilikubali ombi la utetezi, iliamuru Jamhuri kubadili hati ya mashtaka kwa kuwaondoa washtakiwa ambao hawajakamatwa ili haki itetendeke kesi hiyo ianze kusikilizwa.Hata hivyo, Jamhuri uliomba muda wa kumtafuta Poppe na mwenzake ili kesi iendelee.

Nje ya Mahakama

Hans Poppe alifikishwa mahakamani hapo mapema jana saa 2:45 asubuhi na kuwekwa katika mahabusu ya mahakama hiyo hadi saa 11:00 alipopandishwa na wenzake katika ukumbi namba mbili kusikiliza mashtaka yao.

Wanaodaiwa kuwa wadau wa mpira wa miguu walifurika katika viunga hivyo kusikiliza kesi hiyo.

Habari Kubwa