Harakati ukombozi Afrika kuhifadhiwa

18Mar 2019
Na Mwandishi Wetu
TABORA
Nipashe
Harakati ukombozi Afrika kuhifadhiwa

SERIKALI imesema itakarabati maeneo yote ya kihistoria yaliyotumika katika harakati mbalimbali za ukombozi wa Afrika ili kutunza na kuhifadhi kumbukumbu zake.

Mtemi Mirambo wa II (Salumoni Kazikwa) (kulia) akimkabidhi Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Dkt Harrison Mwakyembe (kushoto) vifaa mbalimbali vilivyotumiwa na Shujaa wa Afrika Mashariki na Kati Mtemi Mirambo wakati wa ziara yake jana ya kutembelea maeneo ya urithi wa ukombozi wa bara la Afrika ikiwemo eneo la Shujaa wa Afrika Mashariki na Kati Mtemi Mirambo.

Kauli hiyo ilitolewa jana wilayani Kaliua mkoani Tabora na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, wakati wa ziara ya kutembelea maeneo ya urithi wa ukombozi wa Bara la Afrika likiwamo eneo lenye historia ya makazi ya Shujaa wa Afrika Mashariki na Kati, Mtemi Mirambo.

Waziri huyo alisema lengo la ukarabati huo ambao serikali inaendelea kuutafutia fedha, ni kutunza historia ya mashujaa na maeneo waliyoyatumia na kuwafanya vijana wa sasa na vizazi vijavyo waujue ukweli wa historia za mashujaa wote wa taifa pamoja na wapigania uhuru wa Afrika.

Alisema ukarabati huo unakwenda sambamba na kutafuta kumbukumbu zote walizotumia wapigania uhuru mbalimbali ili kuzitambua na kuzihifadhi rasmi kwa ajili ya vizazi vya sasa na vijavyo na kuendeleza ulinzi wa kazi hizo za kihistoria.

Waziri Mwakyembe alitoa wito kwa Watanzania wote wenye taarifa za kumbukumbu mbalimbali zikiwamo picha, vitabu, mashairi, nyimbo, barua na nyaraka mbalimbali zilizotumiwa na wapigania uhuru wa Tanzania na nje ya nchi, kuziwasilisha Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo au kwa viongozi wa serikali za mitaa ili zitunzwe kwa ajili ya manufaa ya taifa na Afrika.

Aliwataka wananchi na viongozi wa serikali za mitaa kulinda alama zote zilizoko katika maeneo yaliyotumiwa na wapigania uhuru ikiwamo majina katika makaburi na majengo ili kutopoteza kumbukumbu za mashujaa.

Katika hatua nyingine, Waziri Mwakyembe aliwataka wataalamu mbalimbali na maofisa utamaduni nchini, kutumia hazina ya wazee walioko katika maeneo yao wanaojua historia ya kweli kuhusu harakati za kudai uhuru nchini na mapambano ya ukombozi barani Afrika, kupata maelezo na kuyaandika kwa ajili ya kuweka kumbukumbu zake.

“Tunajua kila mtu atakufa, hivyo ni vema tukatumia hazina ya wazee wetu waliopo sasa kupata historia ya kudai uhuru na harakati za ukombozi zilizofanyika nchini ili kuweka kumbukumbu zote zikiwamo picha na maneno yao," waziri huyo aliagiza.

Alisisitiza kuwa simulizi ya wazee ni muhimu katika kuhakikisha hakuna mashujaa walioshiriki harakati za kudai uhuru na ukombozi wa Bara la Afrika zitakazoachwa katika kuandika na kuweka taarifa za kazi zao kihistoria.

Habari Kubwa