Hatima Dk. Shika mikononi mwa DPP

07Dec 2017
Romana Mallya
Nipashe
Hatima Dk. Shika mikononi mwa DPP

HATIMA ya Dk. Louis Shika aliyejizolea umaarufu kwa  kauli ya "900 itapendeza" sasa iko mikononi mwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), imeelezwa.

Dk. Shika aliukwaa umaarufu huo alipotaka kununua nyumba tatu za kifahari za Kampuni ya Lugumi Enteprises kwa thamani ya Sh. bilioni 3.3 Novemba 9, mwaka huu, lakini asimudu kutoa asilimia 25 ya kiasi hicho siku hiyo kama kanuni za minada zinavyotaka.

Mnada huo ulioendeshwa na kampuni ya udalali ya Yono ulihusisha nyumba moja iliyoko Mtaa wa Mazengo, Upanga katika Manispaa ya Ilala na mbili zilizoko jirani na Kambi ya Mbweni JKT, Manispaa ya Kinondoni.

Nipashe jana ilizungumza na Kamanda wa Kanda Maalum ya Polisi Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, kutaka kujua hatima ya Dk. Shika baada ya kumuachia kwa dhamana ya kujidhamini mwenyewe katikati ya mwezi uliopita, lakini alisema jalada lake liko kwa DPP.

"Ukiona kesi haijafikishwa mahakamani ujue haina maslahi kwa umma, na unajua wakati wa mnada wa nyumba zile hapakuwa na madhara yaliyotokea na kwa sababu nyumba za Lugumi zipo na hazijatapeliwa,  ule ulikuwa kama mchezo wa kushinda tu," alisema Mambosasa.

Aidha, Kamanda Mambosasa alisema kutokana na udogo wa kosa lenyewe ndiyo sababu aliamua Dk. Shika ajidhamini mwenyewe baada ya kukaa rumande kwa siku sita na kukosa mtu wa kumdhamini.

"Kwa hiyo kosa ni dogo, lakini tukipata jalada la kesi kutoka kwa DPP basi atafikishwa mahakamani. Mkiona kimya jalada halijatoka maana yake hakuna kosa hivyo hakutakuwa na kesi."

Novemba 9, Dk. Shika alikuwa miongoni mwa washiriki kwenye mnada wa kununua nyumba za Lugumi zilizokuwa zikipigwa mnada na Kampuni ya udalali ya Yono, lakini aliposhindwa kutoa asilimia 25 ya malipo kama masharti ya mnada yanavyotaka na badala yake kudai fedha zake zipo nje ya nchi, ndipo polisi ilipomkamata.

MNADA ULIVYOKUWA

Mkurugenzi wa Yono, Scholastica Kevela, alianza kunadi nyumba hizo na Dk. Shika akiwa miongoni mwa wateja wanaowania kuzinunua.

Wakati wateja wengine wakitaja bei ya kununua nyumba hizo, Dk. Shika naye alikuwa akipanda bei na kuwaacha wanunuzi wenzake kwa mbali hali iliyofanya wafanyakazi wa Yono kumpepea na kumshangilia.

Wakati mnada ukiendelea mnunuzi mmoja alitaja milioni 700 na kupanda hadi milioni 750, Dk. Shika akataja 800. Mwingine alipotaja milioni 810, Dk. Shika ndipo aliposema "900 itapendeza."

Picha kwenye mitandao ya kijamii ziliwaonyesha wafanyakazi wa Yono wakimpepea kwa vitambaa na vipeperushi mbalimbali Dk. Shika wakiamini kuwa yeye ndiye mteja aliyeshinda wenzake na kutwaa nyumba hizo.

Lakini alipotakiwa kutoa asilimia 25 ya fedha za nyumba mbili alizoshinda Mbweni, Dk. Shika ndipo alipowaacha midomo wazi wapiga mnada na washindani wake.

Badala ya kulipa kiasi hicho cha utangulizi, Dk. Shika alisema hakuwa na kiasi hicho cha fedha kwa wakati huo ila angeweza kutoa siku moja au mbili mbele kwa sababu hatembei na fedha kamili mfukoni.

"Tatizo ni kutoelewana, nyumba zinauzwa na wametaka asilimia 25 zilipwe siku hapohapo na mimi fedha zangu zipo nje, hapo ndipo tuliposhindwana," alisema Dk. Shika.

Baada ya kuonekana amevuruga mnada huo, Jeshi la Polisi lilimkamata, kumuhoji na kumweka mahabusu kwa siku sita na baada ya kuona hakuna aliyefika kumdhamini, Kamanda Mambosasa alimtaka ajidhamini mwenyewe.

Kauli yake ya "900 itapendeza" imemfanya kuwa maarufu kiasi cha kupata mialiko kwenye sherehe mbalimbali, yakiwamo matamasha na mikataba kwenye kampuni za matangazo.

Habari Kubwa