Hatima kesi ya Shamim yasubiri ripoti uchunguzi

25Jun 2019
Hellen Mwango
Dar es Salaam
Nipashe
Hatima kesi ya Shamim yasubiri ripoti uchunguzi

UPANDE wa Jamhuri umedai mahakamani katika kesi inayomkabili mmiliki wa Blog 8020 Fashion, Shamim Mwasha (41) na mume wake, Abdul Nsembo(45) ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya Heroin Hydrochloride unasubiri ripoti ya uchunguzi kutoka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali.

Shamim Mwasha AKIWA MAHAKAMANI.

Aidha, umedai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kwamba ripoti hiyo ikiwa tayari, Jamhuri utaijulisha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Madai hayo yalitolewa jana na Wakili wa Serikali, Wankyo Simon, mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Mfawidhi, Kelvini  Mhina.

Wankyo alidai kuwa kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya kutajwa na kwamba upelelezi wake haujakamilika na bado wanasubiri ripoti ya uchunguzi kutoka kwa Mkemia Mkuu.

Hata hivyo, Wakili wa Utetezi, Charles Kisoka, alidai kuwa kesi hiyo haina dhamana, hivyo kuomba upande wa Jamhuri kuharakisha upelelezi ikiwamo kufuatilia ripoti hiyo.

Hakimu Mhina alisema kesi hiyo itatajwa tena Julai 8, mwaka huu, na kuamuru washtakiwa warudishwe rumande.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa hao wanadaiwa kusafirisha dawa hizo za kulevya, Mei Mosi, mwaka huu,  wakiwa eneo la Mbezi Beach,  Kinondoni, jijini  Dar es Salaam kinyume cha sheria ya uhujumu uchumi.

Habari Kubwa