Hatima ya Mbowe bado kitendawili

26Jul 2021
Richard Makore
Mwanza
Nipashe
Hatima ya Mbowe bado kitendawili

HATIMA ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, haitajulikana kutokana na Jeshi la Polisi mkoani Mwanza kutoweka wazi lini atarejeshwa kwa ajili ya kuhojiwa kama lilivyoahidi awali.

Wiki iliyopita Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ramadhani Ng'anzi, alithibitisha kwamba walimkamata Mbowe alfajiri ya Jumatano na kumsafirisha kwenda Dar es Salaam kwa mahojiano kwa makosa mengine aliyokuwa akituhumiwa nayo.
 
Akizungumza na waandishi wa habari siku hiyo, alisema Mbowe baada ya kumaliza kuhojiwa Dar es Salaam angerudishwa jijini Mwanza kwa ajili ya kuhojiwa na jeshi hilo.
 
“Suala la Mbowe bado linashughulikiwa Dar es Salaam, lakini sijajua ni lini atarudishwa, wao (Dar) ndiyo watasema,” alisema.
 
Aidha, taarifa ya maandishi iliyotolewa siku hiyo haikuwa na jina la Mbowe halikuwamo kama mtuhumiwa aliyekamatwa jijini Mwanza pamoja na viongozi wenzake na wanachama.
 
Jeshi hilo lilisema siku ya Jumatano lilikamata watu 15 ambao ni viongozi na wafuasi wa CHADEMA jijini Mwanza kwa madai ya kutaka kufanya mikusanyiko ya kudai ya katiba mpya iliyopigwa marufuku na serikali.
 
Wafuasi na viongozi hao 15 wa CHADEMA baada ya kukaa mahabusu kwa siku tatu, Jumamosi waliachiwa bila kuambiwa ni lini watatakiwa kuripoti tena Polisi.
 
Alisema waliachiwa hadi upelelezi utakapokamilika watawaita tena ili kuwafikisha mahakamani, ingawa hakusema ni lini.
 
Wiki iliyopita msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime, alisema Mbowe anakabiliwa na makosa ya ugaidi ya kupanga njama za kuua viongozi wa serikali.
 
Alipotafutwa jana kwa njia ya simu kuzungumzia kinachoendelea kuhusu Mbowe, pamoja na Kamanda wa Kanda Maalum, Jumanne Muliro, simu zao ziliita bila kupokelewa.

Habari Kubwa