Hatima ya Mdee Aprili Mosi

21Feb 2020
Hellen Mwango
Dar es Salaam
Nipashe
Hatima ya Mdee Aprili Mosi

HATIMA ya Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, anayekabiliwa na kesi ya uchochezi kujulikana Aprili Mosi kama ana kesi ya kujibu au la.

Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, picha mtandao

Hatua hiyo imefikiwa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, iliyoketi chini ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, baada ya upande wa Jamhuri kufunga ushahidi wao.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon, alidai kuwa kesi hiyo imepangwa kwa ajili ya kusikilizwa, lakini upande wa Jamhuri umefunga ushahidi wao na kwamba mashahidi watatu wanatosha kujenga kesi yao.

Hakimu Simba alisema upande wa utetezi uwasilishe hoja zao ndani ya siku 14 na upande wa Jamhuri uwasilishe majibu baada ya siku 14 nyingine.

Alisema mahakama yake itatoa uamuzi wa kama kigogo huyo wa kitaifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Mdee ana kesi ya kujibu au la Aprili Mosi.

Mapema mahakamani hapo, mashahidi watatu wa upande wa Jamhuri wametoa ushahidi akiwamo Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Urafiki, Mrakibu wa Polisi (SP) Batseba Kasanga.

Katika kesi ya msingi, ilidaiwa kuwa Julai 3, 2017 katika Makao Makuu ya Ofisi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), iliyopo Mtaa wa Ufipa Wilaya ya Kinondoni, Mdee anadaiwa kutamka maneno dhidi ya Rais John Magufuli kuwa “anaongea ovyo ovyo, anatakiwa afungwe breki” kwamba kitendo ambacho kingeweza kusababisha uvunjifu wa amani.

Mdee alifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza na kusomewa mashtaka yake Julai 10, 2017 na yupo nje kwa dhamana.

Habari Kubwa