Hatimaye Mwijako apata dhamana

04Aug 2020
Hellen Mwango
Dar es Salaam
Nipashe
Hatimaye Mwijako apata dhamana

HATAMAYE msanii na Ofisa Masoko wa Clouds, Mwemba Burton, maarufu Mwijako (35), anayekabiliwa na mashtaka ya kusambaza picha za ngono kupitia mtandao wa WhatsApp, jana ametimiza masharti ya dhamana na ameachiwa na mahakama.

Dhamana hiyo imetolewa baada ya wadhamini Soud Kafio na Charles Mwendo, kufika jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, iliyoketi chini ya Hakimu Mkazi Mkuu, Richard Kabate.

Hakimu alisema mshtakiwa ametimiza masharti ya dhamana na kwamba jukumu la wadhamini ni kuhakikisha anafika mahakamani kila kesi inapopangwa.

Alisema mshtakiwa yuko nje kwa dhamana mpaka Agosti 12, mwaka huu, kesi yake itakapotajwa.

Julai 29, mwaka huu upande wa Jamhuri ukiongozwa na mawakili wa Serikali Waandamizi, Wankyo Simon na Mwanaamina Kombakono, ulimsomea mshtakiwa mashtaka yake.

Kombakono alidai kuwa kati ya Septamba 17 na Oktoba 10, 2019, mshtakiwa alisambaza picha za ngono kupitia mtandao wa WhatsApp.

Mshtakiwa alikana shtaka hilo.

Wankyo alidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo uko mwishoni kukamilika na sehemu kubwa umeshakamilika.

Alidai kuwa Jamhuri haina pingamizi la dhamana, lakini waliomba mahakama itoe masharti yatakayompa mshtakiwa kuzingatia kufika kwenye kesi yake.

Wiki iliyopita Hakimu Kabate, alisema mahakama yake inampa mshtakiwa dhamana yenye masharti ya heshima na si ya kisaniisanii na kumtaka kuwa na wadhamini wawili kutoka Bongo Muvi au Bongo Fleva wenye barua kutoka Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA).

Habari Kubwa