Hayati Dk. Mengi atunukiwa tuzo

26Oct 2020
Godfrey Mushi
MOSHI
Nipashe
Hayati Dk. Mengi atunukiwa tuzo
  • *Ni kutambua mchango kutokomeza polio, familia kuendeleza hafla chakula kwa wenye ulemavu

FAMILIA ya hayati Dk. Regnald Mengi, imesema kuanzia mwaka ujao itaendelea na utaratibu wa kumwenzi baba yao kwa kuandaa hafla ya chakula cha mchana kwa ajili ya watu wenye ulemavu nchini.

Kaimu Katibu Tawala wa Wilaya ya Moshi, Nathaniel Mshana (kulia), akimkabidhi Mkurugenzi wa Kampuni za IPP, Abdiel Mengi, tuzo ya kutambua mchango wa hayati Dk. Regnald Mengi kwa kuongoza mapambano ya kutokomeza ugonjwa wa polio nchini. Tuzo hiyo ilitolewa juzi na Rotary International kupitia Rotary Club ya Moshi. PICHA: GODFREY MUSHI

Pia, imefafanua kuwa suala la chakula cha mchana kwa watu wenye ulemavu lilikuwa likitekelezwa kama ilivyokuwa desturi miaka yote, Mei 28, mwaka huu, lakini kwa bahati mbaya lilijitokeza tishio la ugonjwa wa virusi vya corona.

Mkurugenzi wa Kampuni ya IPP, Abdiel Mengi, alisema ombi la watu wenye ulemavu kutamani utamaduni huo wa baba yao uenziwe, tayari limeshafanyiwa kazi na Mungu akiwajalia wataendelea nalo mwaka 2021.

Alikuwa akizungumza juzi na watu mbalimbali mjini Moshi, wakati wa hafla ya kupokea tuzo ya ‘Paul Harris Fellow Major Donour’ iliyotolewa kwa baba yake na Rotary Foundation of Rotary International, kwa ajili ya kutambua mchango wa Dk. Mengi katika kutokomeza ugonjwa wa polio nchini.

 

Kuna hoja moja aliitoa hapa mzee Elimringi Ngowi: “Nikuhakikishie, mzee (Mengi) hajafa. Kimwili ndio! Kiroho bado yupo. Kama ulivyosema yuko duniani na kupitia kizazi chake na kupitia ndugu, jamaa na marafiki, wote aliowaacha, spirit (roho) yake bado tunaendelea nayo.

“Suala la lunch (chakula) ya wenye ulemavu, lilikuwa litekelezeke kama desturi ilivyokuwa miaka yote, unfortunately (bahati mbaya) mwaka jana tulikuwa tumepanga tuifanye tarehe 28 Mei mwaka huu, na tulikuwa tumeshatangaza kwa viongozi wa taasisi mbalimbali za watu wenye ulemavu, walikuwa wameshapata hiyo taarifa.

“Lakini likaja suala la corona na tukaona mfano kuanzia serikalini, wanasimamisha hadi mbio za Mwenge wa Uhuru na ukishaona hizo dalili ujue situation (hali) ishakuwa serious (mbaya).

“Kwa hiyo tusingeweza kufanya lolote lile kwa muda huo na kuhatarisha maisha ya wenzetu. Ndio maana mwaka jana hukusikia. Lakini mwaka huu tayari limeshafanyiwa kazi. Mwenyenzi Mungu akitujalia mwaka huo unaokuja tutaendelea.”

Akishukuru kwa kukabidhiwa tuzo hiyo, Abdiel, alisema  familia wanamshukuru mwenyenzi Mungu, kwa kuwa na baba kama Regnald Mengi, kwa sababu alikuwa na vitu vingi sana kwao, na hawana zaidi ya kumshukuru Mungu, kwa namna alivyoweza kumjalia baba yao kuwa na utu unaojali binadamu.

“Na kwa hilo nadhani ni talanta kutoka kwa mwenyenzi Mungu na kila siku tunashukuru kwa kuweza kuwa pembeni yake, kuwa naye, kuwa nyuma yake. Kuna jinsi alivyokuwa anaweza kuitumia hiyo talanta.

“Siku ya leo kupata hii kumbukumbu ni siku ambayo pia inatukumbusha kitu kingine pengine sisi kama wanafamilia. Ni siku ambayo inatukumbusha pia kusema asante kwa mwenyenzi Mungu na kumwombea sala baba yetu, kwa sababu yote haya tunayapata kwa ajili yake.

“Dk. Regnald Mengi alifanya vitu vingi sana katika maisha yake yote, lakini asingeweza kufanya vitu vyote mwenyewe, nyuma yake na pembeni yake alikuwa na watu, alikuwa na taasisi kama hii Rotary Club, ambao pamoja walikuwa wanatiana moyo katika suala zima la kushughulikia changamoto zinazoikabili jamii zetu.”

 

 “Niseme tu Rotary mmepiga hatua kubwa sana katika suala zima la kuondoa unnecessary human suffering (kuondoa matatizo yanayowakabili binadamu), hasa suala zima la kuondoa na kufanya ugonjwa wa polio na madhara yake kuonekana katika vitabu vyetu vya historia) ni hatua kubwa sana. Napenda niwapongeze kwa sababu maisha bila polio na hata maradhi mengine kupungua, hayo ni maisha mazuri. Hongereni sana kwa hilo na mafanikio makubwa.”

Awali, Rais Rotary Club ya Moshi, Cynthia Asiyo, alisema tuzo hiyo imetolewa kwa niaba ya wanachama wa Rotary Club milioni 1.2 duniani kote, kutambua mchango mkubwa wa Dk. Mengi alioufanya na kuifanya Afrika kuwa haina polio.

Kwa mujibu wa rais huyo, Machi 18, mwaka 2011, Dk. Mengi aliongoza matembezi ya hisani yaliyohusisha mamia ya watu, baada ya kuandaliwa na Rotary Club ya Moshi kuzunguka viunga vya manispaa hiyo na kuchangia peke yake Sh. milioni 40.

Alifafanua kuwa baada ya mchango wa Dk. Mengi, baada ya wiki nane kupita, Afrika nzima ilitangazwa haina ugonjwa wa polio, ndio maana leo wanachama wa Rotary kila mahali na asilimia 90 ya watu wenye utu wote wanamkumbuka Mengi na washirika wake duniani kwa kuondoa ugonjwa huo.

Mkurugenzi wa maduka ya dawa baridi ya binadamu ya Kilimanjaro Pharmacy, Arthur Kiwia, akisoma taarifa ya Siku ya Polio Duniani iliyoandaliwa na Rotary ya Moshi, alisema Tanzania kwa sasa ina club 50 zenye wanachama 750.

Habari Kubwa