Heche alalamikia polisi kuzuia mikutano yake

19Jul 2019
Enock Charles
Dar es Salaam
Nipashe
Heche alalamikia polisi kuzuia mikutano yake

MBUNGE wa Tarime Vijijini (Chadema), John Heche, amelilalamikia Jeshi la Polisi Mkoa wa Mara kwa kumzuia kufanya mikutano ya kisiasa na wananchi jimboni kwake.

MBUNGE wa Tarime Vijijini (Chadema), John Heche.

Akizungumza na Nipashe kwa simu jana, Heche alisema Jeshi la Polisi mkoani humo limemzuia kufanya mikutano licha ya kutoa taarifa kwa jeshi hilo kila wakati anapotaka kufanya mikutano.

“Siwaelewi na hawana sababu za msingi za kunizuia mimi kama mbunge kufanya mikutano katika jimbo langu, niliongea na RPC anadai wananipa adhabu kwa kuwa kipindi Ester Matiko ametoka gerezani nilienda kufanya mkutano jimboni kwake,” alisema Heche.

Awali, ulisambaa ujumbe wa video kwenye mitandao ya kijamii ukimwonyesha mbunge huyo akivutana na polisi na baadaye andiko la mbunge huyo akilalamikia polisi mkoani humo.

Gazeti hili lilimtafuta Kamanda wa Polisi mkoani humo, Henry Mwaibambe, kujua ukweli kuhusu lawama hizo za mbunge kwa Jeshi la Polisi, lakini simu yake iliita bila kupokelewa na alipotumiwa ujumbe mfupi wa maandishi alijibu kwa kifupi kuwa ni kweli mbunge huyo alikiuka taratibu lakini hakufafanua taratibu hizo.

“Ni kweli kuna taratibu alikiuka tumeshamwambia,” Kamanda Mwaibambe alijibu kwa kifupi.

Akizungumza na askari kwenye ziara yake ya kikazi mkoani Tabora jana, Mkuu wa Jeshi la Polisi, (IGP) Simon Sirro, alisema hawajakataza mikutano ya ndani wala ile ya wabunge kwenye majimbo yao.

Simon Sirro alisema mikutano ya ndani ya vyama vya siasa haijapigwa marufuku kama inavyozungumzwa.

Akizungumza na askari kwenye ziara yake ya kikazi mkoani Tabora juzi, IGP Sirro alisema mikutano hiyo inaweza kusitishwa tu pale itakapoonekana kwamba kuna viashiria vya uvunjifu wa amani.

“Mikutano ya ndani halijapigwa marufuku popote ila kama kuna taarifa za tishio la usalama kwenye mkutano huo tunaweza kuzuia kwa faida ya Watanzania,” alisema

IGP Sirro kuwa mikutano hiyo inaruhusiwa kunapokuwa na mazingira ya amani na kwamba wahusika wanachotakiwa kuzingatia ni kufuata sheria na taratibu zilizowekwa kila wakati.

“Tunapokuwa tumezuia mikutano ya ndani watu wazingatie sheria na watii kwa sababu askari wanakuwa na taarifa zinazoweza kusababisha vurugu sasa tunawataka wahusika watii amri za polisi,” alisema IGP Sirro.

Habari Kubwa