HESLB yawataka wanafunzi wanaodaiwa kurejesha mikopo

15Feb 2021
Dotto Lameck
Arusha
Nipashe
HESLB yawataka wanafunzi wanaodaiwa kurejesha mikopo

BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), imewataka wanufaika waliohitimu katika Vyuo vikuu na Taasisi mbalimbali za Elimu ya juu nchini kurejesha Mikopo yao ili iweze kuwasaidia kukopesha wengine wanaojiunga na elimu ya juu.

Akizungumza wakati wa kufungwa kwa Maonesho ya Nne ya Mifuko na Programu za kuwawezesha Wananchi Jijini Arusha, Meneja wa HESLB Kanda ya Kaskazini - Arusha Patrick Shoo, amesema wahitimu wa elimu ya juu wanaweza kurejesha Mikopo yao kidogo kidogo hata kama wamejiajiri wenyewe kwenye ujasiriamali.

Amesema katika kipindi cha siku saba za maonesho hayo wameweza kukutana na wajasiriamali kadhaa waliojitokeza kwenye Banda lao na kupata taarifa za madeni yao na wengine kulipa kwa njia ya simu.

"Kwenye maonesho haya tumeweza kukutana na wadaiwa waliopo kwenye Sekta isiyo rasmi ambao ni wajasiriamali na tumeweza kuwapa taarifa za madeni yao na wengine wamelipa kwa njia ya simu", amesema Shoo.

Aidha Shoo amesema kuwa wahitimu wengi huwa wanakaa kimya kwa kigezo cha kutokuwa na ajira huku wakijihusisha na ujasiriamali na kwamba wanaweza kujipanga katika kipato wanachopata kwa kujiwekea utaratibu wa kulipa taratibu hata kwa njia ya simu.

"Kitu kikubwa kwa wanufaika wetu ni kupata taarifa za madeni yao ili waweze kulipa taratibu kulingana na kipato chao. Hapa tumeweza kutoa taarifa za madeni ya wahitimu lakini pia wazazi na wanafunzi tumeweza kuwapa elimu ya namna ya kuomba mikopo kwa usahihi," ameongeza.

Habari Kubwa