HESLB yatunuku waajiri 12 urejeshaji mikopo

28Feb 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
HESLB yatunuku waajiri 12 urejeshaji mikopo

BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), imetoa tuzo kwa waajiri 12 kutoka Arusha na Kilimanjaro kwa kufanikisha kila mwezi kukata makato ya mikopo ya wanufaika na kuirejesha kwa bodi hiyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru, PICHA MTANDAO

Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru, alisema kwa mwaka 2017/18, waajiri sita kutoka Mkoa wa Arusha waliwasilisha makato ya Sh. milioni 74.08 kwa wanufaika 410 wa mikopo hiyo.

Hata hivyo, alisema makusanyo kutoka kwa wanufaika wote mkoani Arusha kwa mwaka 2017/18 ni Sh. bilioni 2.8 kutoka sekta binafsi.

Kwa upande wa Mkoa wa Kilimanjaro, alisema, walikusanya Sh. milioni 23.866 kutoka kwa wanufaika 142 kwa mwaka 2017/18 na kwamba makusanyo yote katika kipindi hicho kutoka sekta binafsi yalikuwa Sh. bilioni 1.1.

Badru, alisema waajiri hao wametoa mchango mkubwa wa kuwasilisha makato ya asilimia 15 ya mshahara ghafi wa waajiriwa wao kabla ya tarehe 15 ya mwezi unaofuata.

Pia alisema wamekuwa wakiijulisha Bodi iwapo wafanyakazi wanufaika wa mkopo wameacha kazi au kama wamefariki.

"Waajiri hawa wamekuwa wakiwasilisha majina ya wafanyakazi wenye kiwango cha elimu ya shahada na stashahada ndani ya siku 28 tangu waajiriwe na wamekuwa wakitoa ushirikiano kwa watumishi wa Bodi pindi inapohitaji kufanya hivyo (ukaguzi)," alisema.

Taasisi na kampuni zilizotunukiwa tuzo kutoka Arusha na kiasi cha fedha kwenye mabano ni World Vision Tanzania (Sh. milioni 19.03) ikiwa na wanufaika 97, Shirika la Hifadhi za Taifa (Sh. milioni 17.6) ikiwa na wanufaika 45 na Kampuni ya Off-Grid Electric–ZOLA (Sh. milioni 17.46) ikiwa na wanufaika 117.

Mengine ni Vision Fund Tanzania (Sh. milioni 10.45) ikiwa na wanufaika 69, The School of St Jude (Sh. milioni 8.2) ikiwa na wanufaika 59 na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira- AUWSA (Sh. milioni 4.4) ikiwa na wanufaika 23.

Kutoka Kilimanjaro yaliopewa tuzo ni Kilimanjaro Airport Development Company-Kadco (Sh. milioni 6.38) ikiwa na wanufaika 34, Mwenge Catholic University (Sh. milioni 6.05) ikiwa na wanufaika 32, Tanganyika Planting Company Ltd (Sh. milioni 4.3) ikiwa na wanufaika 20, Bonite Bottlers Ltd (Sh. milioni 3.9) ikiwa na wanufaika 34, Marenga Investment Ltd (Sh. milioni 2.3) ikiwa na wanufaika 15 na Uchumi Commercial Bank (Sh. milioni 0.936) ikiwa na wanufaika saba.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Gambo, aliiomba Bodi hiyo kuangalia mazingira na hali ya waombaji wakati wa mchakato wa kuomba mkopo.

Alisema wapo wazazi waliokuwa na uwezo kusomesha watoto wao shule binafsi kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha sita, lakini baada ya hapo wakakabiliwa na changamoto za kikazi au biashara na hivyo kuwafanya wasiwe na uwezo tena wa kuwasomesha.

"Mzazi alikuwa na uwezo, lakini baadaye zikajitokeza changamoto kiasi cha kumfanya asiwe na uwezo huo, Bodi inaweza kuangalia hilo kwa kuwa uwezo wa mzazi haupo tena wakati huo.

"Hawana tena uwezo wa kuendelea kuwasomesha kutokana na changamoto kazini, kama vile kufukuzwa kazi au kukosa biashara," alisema.

Habari Kubwa