HESLB yawapa mbinu wastaafu makato mafao

05Jul 2019
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe
HESLB yawapa mbinu wastaafu makato mafao

BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), imewataka wastaafu watarajiwa wanaodaiwa mikopo wailipe kwa utaratibu wa kawaida, badala ya kusubiri hadi kustaafu, hivyo kusababisha kiinua mgongo chao kikatwe.

bodi ya mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB).

Mkurugenzi wa msaidizi Urejeshaji wa Mikopo kutoka HESLB, Fidelis Joseph, alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumzia ujereshaji mikopo kwa wanufaika akiwa kwenye kipindi cha East Africa Breakfast cha East Africa Radio,

Akizungumza kwenye kipindi hicho, Joseph alisema taratibu za kuwafuata wastaafu ni za kawaida na kwamba bodi haiendi kuchukua kiinua mgongo chao chote bali kumpa taarifa mhusika kuwa anadaiwa.

“Kwa hiyo atakuwa ana jukumu la kulipa deni hadi liishe. Deni litakuwa limeisha pale utakapokuwa umekufa au ukipata matatizo ya kudumu kama ugonjwa kwa hiyo kama ni mstaafu lazima ulipe deni kwa nia yeyote,” alisema.

Akielezea kuhusiana na ongezeko la deni la bodi hiyo kwa wanafunzi kila mwaka kama ambavyo imekuwa ikidaiwa na wanufaika, Fidelis alisema wamewekewa sheria ambayo lengo lake ni kulinda thamani ya fedha kwa watu ambao wanachelewesha.

“Madeni ya serikali hayana riba, ila yana tozo ili kulinda thamani ya fedha mfano kama unadaiwa Sh. milioni 10 utalipa Sh. milioni 10.6 na kama ulilipa Sh. milioni 5 ukifika mwisho wa mwaka unadaiwa asilimia 6 ya Sh. milioni 5, lengo lake ni kweli kwamba fedha huwa inabadilika thamani lakini siyo kweli kwamba deni la bodi huwa haliishi,” alisema.

Meneja wa Habari, Elimu na Mawasiliano wa bodi hiyo, Omega Ngole, aliliambia Nipashe kuwa HESLB haikopeshi mkopo mtu mwenye umri zaidi ya miaka 35, hivyo hata kama mtu atasoma taaluma ambayo inachukua miaka mitano kama udaktari akiwa na umri huo, hadi anamaliza atakuwa na miaka 40 au 41.

“Kama mtu amemaliza chuo akiwa na umri huo tunamshauri ni vyema alipe mkopo wake mapema kwa sababu kadri unavyoendelea kuuacha kuna penati, kwa nini usubiri hadi ustaafu ndo uanze kukatwa, lipa mapema na hutakumbana na penati, lipa ili kuruhusu wengine nao wanufaike na mikopo tunayotoa,” alisema.

Aliongeza kuwa, “Ukimaliza chuo lipa mkopo wako, usisubiri hadi utafutwe. Ukikimbia utakutana na penati kwenye mkopo uliokopa, ukistaafu ujue tutakupata tu,” alisema.

Bodi ya Mikopo ilianzishwa kwa sheria ya Bunge namba 9 ya mwaka 2004 na kuanza rasmi mwezi Julai 2005 kwa majukumu ya kutoa mikopo kwa wanafunzi wahitaji waliodahiliwa katika Taasisi za Elimu ya Juu pamoja kukusanya marejesho ya mikopo yote iliyotolewa tangu mwaka 1994.

Hadi mwezi Machi mwaka huu Bodi hiyo ilikuwa imekusanya zaidi ya Sh. bilioni 120 kutoka kwa wanufaika wa mikopo nchini, ikiwa ni madeni ya miezi minane.

Akizungumza Machi mwaka huu jijini Dodoma, Mkurugenzi wa Ukusanyaji Mikopo wa HESLB, Ignatus Oscar, alisema bodi ilipanga kukusanya zaidi ya Sh. Bilioni 180 ifikapo mwezi Juni mwaka huu.