Hivi ndivyo kodi laini za simu itakavyotozwa

17Jun 2021
Augusta Njoji
Dodoma
Nipashe
Hivi ndivyo kodi laini za simu itakavyotozwa

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba, amelazimika kutoa ufafanuzi kuhusu makato ya kodi kupitia miamala ya simu, huku akiweka wazi kuwa mtumiaji atakatwa mara moja kwa vocha atakayoweka na si kwa simu kama inavyodaiwa.

Mwigulu alilazimika kutoa ufafanuzi huo jana kwenye Mkutano wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Taasisi zake na Wahariri wa Vyombo vya Habari jijini hapa.

Alisema kuanzia Sh. 100,000 kwenda juu anatozwa Sh. 200 na sio kila siku, na ni pale anapoweka, Sh. 0,000 hadi 100,000 anatozwa Sh. 180 huku, Sh.2,500-5,000 atatozwa Sh. 21.

“Kia mfano, mimi kwenye laini yangu ya Halotel kuna kifurushi kinaitwa Tanzanite unaipa Sh. 50,000 kwa mwezi maana yake kwenye kiasi hicho kwa mwezi nitakatwa Sh. 180. Hivi kwa vifo vya mama zetu mtu unayeweka 50,000 ukatozwa hiyo fedha kuokoa maisha yao kwenye kuboresha huduma kuna shida gani, nikaweka TTCL wakanitoza Sh. 100 kwa mwezi."

“Nimeona watu wanachanganya hata kule bungeni wanasema sasa kila siku itakuwa inakatwa Sh. 10 hadi 200 kila siku, wanasema hata kama hukuweka vocha inakuwa kama ile ya nipige tafu, hatukuweka hivyo na wala hatujaweka Sim Card Tax, tulichoweka ule ni uwiano tu tunasema kwa mtu ambaye anaweka kuanzia Sh. 1,000 hadi 2,500 pale anapoweka ndio anatozwa Sh. 10, inayotajwa ni Sh. 200 inaonekana bibi wa kijijini huko anakwenda kukatwa Sh. 200, sio kweli,” alisema.
Waziri huyo alisema makato hayo ni pale mtu anapoweka vocha sio kama anavyopiga.

Kuhusu miamala ya kutuma fedha, Mwigulu alisema kwa Sh. 1,000 hadi 2,000 atatozwa Sh. 10, Sh. 10,000 hadi 15,000 anatozwa Sh. 300 kwa muamala wa Sh. 30,000 na kuendelea atatozwa Sh.1,000 huku kuanzia Sh. milioni tano na kuendelea atatozwa Sh. 10,000.

“Sio kwamba Sh. 10 ni mzigo na sio kwamba siwahurumii Watanzania, lakini tukapima shida walizo nazo Watanzania, maendeleo ya nchi yetu yatajengwa na Watanzania wenyewe,” alisema.

Kuhusu mfumo wa ulipaji kodi, alisema kuna maeneo kuna shida na kwamba kwa miaka yote walipakodi waliosajiliwa wapo chini ya milioni tatu na walipakodi wakubwa wapo kati ya 400-500.

“Hatukimbilii kupandisha kodi kwa kuwa kodi zingine zinaua ajira na kukimbiza wawekezaji na kuua sekta binafsi, kuna miradi mikubwa inahitaji fedha tutawaunganisha wapi Watanzania pamoja, wakiwa wengi tunapunguza mzigo, tunagawanya huu mzigo hili jukumu ni la Watanzania wenyewe,” alisema.

Akizungumzia makato ya Sh. 100 kwa lita ya mafuta ya petroli na dizeli, Mwigulu alisema kodi hiyo ambayo imeongezeka serikali itapeleka fedha hizo kama ilivyoeleza kwenye bajeti kwamba zitapelekwa TARURA kwa ajili ya ujenzi wa barabara ambazo nyingi ni mbovu na kusababisha adha kubwa kwa wananchi ambao wanahitaji huduma mbalimbali za kijamii.

Habari Kubwa