Hofu yatanda ng’ombe kuchinjwa kwa misumeno

22May 2022
Gideon Mwakanosya
Songea
Nipashe Jumapili
Hofu yatanda ng’ombe kuchinjwa kwa misumeno

​​​​​​​Wananchi wa Manispaa ya Songea, wamekumbwa na hofu kuhusu usalama wa nyama wanayokula baada ya kuwapo madai kuwa ng’ombe katika machinjio ya Shule ya Tanga, wanachinjwa kwa kutumia misumeno.

Hata hivyo, Mkurugenzi  wa Manispaa ya Songea, Dk. Francis Sagamiko, amewaondoa hofu wakazi wa manispaa hiyo akisema sikweli kwamba mifugo katika machinjio ya Shule ya Tanga inachinjwa kwa kutumia misumeno ya kupasulia mbao.

Akizungumza na Nipashe, Dk. Sagamiko alisema mfumo unaotumika katika machinjio hayo ni wa kisasa na kwamba unafanyakazi vizuri.

Mkurugenzi huyo aliwatoa hofu wananchi kuwa nyama zinazotoka katika machinjio hiyo ni halali ni tofauti na taarifa zilizo zagaa ambazo zimeonyesha kutaka kuichafua serikali.

Juzi, Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Manispaa ya Songea likiongozwa na Meya, Michael Mbano, baadhi ya madiwani walisema mashine za kuchinjia nyama katika machinjio ya Shule ya Tanga hazifanyi kazi na badala yake wamekuwa wakitumia mashine za kupasulia mbao kuchinjia mifugo.

Hali hiyo ilisababisha taharuki kwa wakazi wa Manispaa ya Songea.

Wakizungumza na Nipashe kwa nyakati tofauti, wakazi wa mji wa Songea walidai kuwa kwa muda mrefu tangu machinjio hiyo ijengwe na kuanza kazi wamekuwa wakiamini kuwa wanyama wanaochinjwa kwenye machinjio hiyo wanachinjwa kitaalamu kwa kutumia mitambo ya kisasa iliyopo kwenye machinjio hiyo.

Walisema wameshtushwa na taarifa zilizotolewa na madiwani kwamba mifugo katika machinjio hiyo imekuwa ikichinjwa kwa kutumia misumeno ya kupasulia mbao.

Stephan Komba, Mkazi wa Bombambili Manispaa ya Songea, aliiomba serikali kupitia Mkuu wa Wilaya kuchukua hatua za haraka ili kuona namna ya kumaliza matatizo yaliyopo kwenye machinjio hiyo.

Hussein Ngonyani, Mkazi wa Mshangano katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea alisema taarifa aliyoisikia kupitia vyombo vya habari kuhusu machinjio hayo imemsikitisha.

Akizungumza na Nipashe, Dk. Sagamiko alisema: “Siyo kweli kwamba mifugo inachinjwa kwa kutumia misumeno, niwatoe hofu wananchi kwamba nyama inachinjwa kitaalamu na mitambo ya kisasa.”

Msimamizi mkuu wa wafanyabiashara ya maduka ya nyama ya ng’ombe, Andrea Kanuda, alisema taarifa hizo si za kweli, na kwamba machinjio hayo yanatumika kila siku wanachinjwa ng’ombe kwa kutumia mashine za kisasa.

Kanuda alifafanua kuwa mashine zilizopo kwenye machinjio hiyo kwa siku wanachinja ng’ombe kati ya 30 hadi 40 na inategemea na hali ya biashara.

Alisema kuwa wanyama wanachinjwa kwenye machinjio hiyo na Shekhe Issa Chamaja aliyeteuliwa na Baraza la Waislam Tanzania (BAKWATA) Mkoa wa Ruvuma, kwamba siyo kweli  wananchi wanalishwa vibudu.

Msimamizi mkuu wa machinjio ya wanyama, Said Sangija, alisema kwa wastani zaidi ya ng’ombe 40 wanachinjwa kwa siku katika machinjio hayo.

Alisema matatizo yanayotokea katika machinjio hiyo ni ya kawaida na yamekuwa yakitatuliwa.

Diwani wa kata hiyo, Agaton Goliama, alisema taarifa za mifugo kuchinjwa kwa misumeno ya kupasulia mbao siyo za kweli na kwamba zilikuwa na lengo baya.

Habari Kubwa