Hoja 10 zinazosubiri majibu ya Mpango mjadala bajeti

24Jun 2019
Godfrey Mushi
DODOMA
Nipashe
Hoja 10 zinazosubiri majibu ya Mpango mjadala bajeti

HOJA takribani 10 za mjadala wa bajeti kuu ya serikali ya mwaka wa fedha 2019/20, zinasubiri majibu ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, kwa wabunge, ambazo walizoeleza katika michango yao wiki iliyopita.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Phillip Mpango, bungeni jijini Dodoma.

Ziko hoja kadhaa ikiwamo sera ya mwaka jana iliyoruhusu msamaha wa kodi kwa taulo za kike kufutwa na serikali kuja na pendekezo la kurejesha kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwenye taulo za kike.

Masuala mengine yaliyoibuka katika bajeti hiyo ya Sh. trilioni 33.1 ni mazingira ya uendeshaji wa biashara nchini, utitiri wa kodi na tozo zilivyochangia kuua soko la kimataifa la Kariakoo, jijini Dar es Salaam na kupandishwa kwa kodi kwenye nywele za bandia hasa mawigi na rasta za bei mbaya.

Hoja nyingine ni kukua kwa hali ya uchumi visiwani Zanzibar, huku gharama za maisha visiwani humo zikidaiwa kuongezeka kutokana na tozo za kodi za bidhaa zinazoingia kutoka Bara.

Limo pia pendekezo la serikali la kuongeza kodi kwenye mafuta ghafi yanayotoka nje ya nchi ili kulinda wazalishaji wa mbegu za mafuta hapa nchini.

Pia, suala la serikali kutenga fedha nyingi katika miradi mikubwa ya maendeleo na kuacha kutazama sekta ya kilimo inayogusa moja kwa moja maisha ya kila siku ya Mtanzania.

Kwa mujibu wa ratiba ya mkutano wa 15 wa Bunge (mkutano wa bajeti), Waziri Dk. Mpango anapaswa kujibu hoja za wabunge zilizochomoza katika mjadala kuhusu taarifa ya hali ya uchumi, hotuba ya bajeti ya serikali na kuhitimisha mjadala huo leo au kesho ukifuatiwa na upigaji wa kura ya wazi.

Mkutano huo wa Bunge la Bajeti, ulianza Aprili 2, mwaka huu na linatarajiwa kumalizika 28 Juni, 2019 ambapo Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa atatoa hoja ya kuahirisha Bunge.

KUFA KWA SOKO LA KARIAKOO

Pia suala la kupotea katika ramani ya biashara soko la kimataifa la Kariakoo, nalo lilichukua mjadala mpana huku, wabunge wakitaka Waziri Mpango kukaa pamoja na Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa na kutafuta ufumbuzi wa kulirejesha kuwa imara.

Aliyeibua hoja hiyo alikuwa ni Mbunge wa Mvomero (CCM), Sadiq Murad, aliyedai kuwa soko la Kariakoo limepotea katika ramani ya biashara, licha ya kuwa Tanzania ilishafanikiwa kuziteka kibiashara nchi za Burundi, Rwanda, Malawi, Uganda na Kongo.

KUHUSU KILIMO

Katika mjadala huo baadhi ya wabunge, walieleza kuwa kilimo ni sekta inayotakiwa kuguswa kikamilifu ili kupambana na umaskini wa watu, hivyo haikuwa vyema kuitengea kiasi kidogo cha fedha.

Mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye aliyeeleza: “Kilimo kinazalisha ajira asilimia 65 na asilimia 85 ya bidhaa tunazouza nje zinatokana na kilimo. Kilimo kinachangia pato la taifa kwa asilimia 29 na asilimia zaidi ya 100 chakula nchini kinategemea kilimo,”

“Lakini ukiangalia mtiririko wa bajeti mwaka 2016/17 bajeti ya maendeleo katika kilimo tulitenga asilimia 1.38, mwaka 2017/18 tukatenga asilimia 1.25 na 2018/19 tukatenga asilimia 0.81 na 2019/2020 tumetenga asilimia 1.17 na hizi fedha zimetengwa tu bado hazijapelekwa.”

Taulo za kike

Uamuzi wa serikali kurejesha Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye taulo za kike ni moja ya hoja iliyowagusa wabunge karibu wote, lakini kubwa ni Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe, kupinga pendekezo la serikali la kurejesha kodi, akiamini ni uamuzi wa haraka na unaharibu sifa ya Tanzania.

Katika mapendekezo hayo ya bajeti ya Sh. trilioni 33.1, serikali imeweka wazi kuwa ina mpango wa kurejesha VAT kwenye taulo za kike iliyoifuta mwaka jana kwa kuwa uamuzi wake huo haukufanikiwa kupunguza bei ya bidhaa hiyo muhimu.

Baadhi ya wabunge wamedai kuwa serikali ilikuja na pendekezo kwenye Bunge ili kuweza kuleta unafuu kwa wanawake milioni 13 katika matumizi ya taulo za kike kwa kila mwezi na kwa mwaka huu, wanashangaa ni kwa nini serikali imeona kwamba pendekezo lile halijaleta yale matokeo ambayo ilikuwa inayataka.

Kwa upande wake, Mbunge wa Mtwara Vijijini (CCM), Hawa Ghasia, alisema njia pekee ya kumsaidia mwanamke na mtoto wa kike kwenye bidhaa hizo ni serikali kuhakikisha inasimamia viwanda vya ndani ili taulo hizo zizalishwe kwa wingi na kwa bei nafuu.

Mafuta ya kula

Kuhusu pendekezo la serikali la kuongeza kodi kwenye mafuta ghafi yanayotoka nje ya nchi ili kulinda wazalishaji wa mbegu za mafuta hapa nchini, baadhi ya wabunge waliochangia mjadala huo wa bajeti wameeleza kuwa bado uzalishaji unashuka na kuna haja serikali ikafanya mapinduzi zaidi ya kulinda soko.

Gharama za maisha Zanzibar

Katika mjadala huo, baadhi ya wabunge akiwamo Mbunge wa Welezo Zanzibar, Saada Mkuya (CCM) alieleza masikitiko yake kwamba bidhaa zinazoingia kutoka Bara kwenda Zanzibar zinatozwa kodi ya ongezeko la thamani (VAT) na zikifika tena Zanzibar zinatozwa kodi na Mamlaka ya Mapato Zanzibar, jambo linawakwaza wafanyabiashara na kutikisa mitaji yao.

Suala la PPP

Hoja kuhusu ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi lilikuwa miongoni mwa mambo yaliyoguswaguswa na baadhi ya wabunge akiwamo Mbunge wa Momba (Chadema), David Silinde, aliyetaka serikali kutambua kuwa maendeleo ya nchi hayategemei kukusanya kodi.

Alisema maendeleo hutegemea kuboresha uwekezaji wa moja kwa moja na ushirikiano wa sekta binafsi na umma (PPP).

“Duniani kote maendeleo ya nchi hayategemei kodi pekee, nasema hivi kwa sababu wimbo humu ndani (bungeni) ni kodi tu. Nchi nyingi hutumia kodi kwa matumizi mengineyo na kulipa mishahara,” ameeleza Silinde.

Taasisi zenye majukumu yanayofanana

Pamoja na mambo mengine, wakati wa mjadala huo, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti ilitoa mapendekezo yake yaliyogusa wabunge wengi ambao wameitaka serikali iharakishe mchakato wa kuziunganisha taasisi zote zenye majukumu yanayofanana ya ukaguzi kwenye bidhaa, kampuni, taasisi na maeneo ya viwanda nchini ili kuondoa kero na usumbufu unaojitokeza.

Taasisi ambazo Bunge limeekeleza serikali kuziunganisha ni Shirika la Viwango nchini (TBS), Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) na Jeshi la Zimamoto na Uokozi.

Habari Kubwa