Hoja binafsi taulo za kike kutinga bungeni 

23Jan 2018
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Hoja binafsi taulo za kike kutinga bungeni 

MBUNGE wa Viti Maalum (Chadema), Upendo Peneza, amesema anakusudia kuwasilisha hoja binafsi bungeni kuitaka serikali kutoa taulo za kike bure kwenye shule, ili kupunguza utoro wa masomo kwa watoto wa kike. 

Peneza aliyasema hayo katika kongamano la ‘Jitambue Mwanamke’ lililofanyika juzi mjini hapa kwa ajili ya kujadili changamoto zinazowakabili wanawake. Alisema asilimia kubwa ya utoro kwa watoto wa kike shuleni inatokana na wanafunzi wa kike kutohudhuria masomo yao ipasavyo wakati wa hedhi kutokana na kushindwa kujisitiri. Alisema kila mwezi mtoto wa kike hukosa siku tatu za masomo shuleni kutokana na hedhi na kwamba endapo watapata vitaulo vya kujisitiri wataweza kuhudhuria ipasavyo masomo yao. Mbunge huyo alisema atawasilisha hoja hiyo bungeni na kwamba hatua zitakazochukuliwa na serikali zitasaidia kwa kiasi kikubwa kuondokana na tatizo la utoro. “Lengo ni kuona watoto wa kike wanasoma kama ilivyo wa kiume bila kukosa shule kutokana na sababu zisizo za msingi,” alisema. 

Habari Kubwa