Homa ukaguzi miradi ya vyama vya ushirika Siha yapanda

14Jan 2022
Anjela Mhando
SIHA
Nipashe
Homa ukaguzi miradi ya vyama vya ushirika Siha yapanda

HOMA ya ukaguzi wa mali na miradi ya vyama vya ushirika katika Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro, inazidi kupanda baada ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kutangaza nia yake ya kupita chama kimoja hadi kingine kujiridhisha juu ya mwenendo wa vyama hivyo.

Katibu wa CCM wa Wilaya ya Siha, Alli Kidunda.

Katibu wa CCM wa Wilaya ya Siha, Alli Kidunda, alikoleza homa hiyo leo, alipokuwa akizungumza na Nipashe kuhusu ufuatiliaji wa ilani ya chama hicho.

“Ni kweli tumekusudia kufanya ziara wilaya nzima, tukiongozana na maofisa ushirika ili kujua ni nini kinachoendea ndani ya vyama hivyo. Vyama tutakavyotembelea ni vile vya ushirika, Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo (SACCOS) na Vyama vya Ushirika wa Mazao (AMCOS),”amesema

Katika taarifa yake, Kidunda amesema katika wilaya hiyo, hali ya ushirika si ya kuridhisha sana, kwa kuwa licha ya kuwapo hatua iliyopigwa kwenye maendeleo, bado maeneo kadhaa kuna malalamiko ya wananchi.

Kidunda, amesema wao kama chama kinachosimamia utekelezaji wa ilani, watapita kijiji kwa kijiji na kukutana na viongozi wa vyama vya msingi, vyama vya ushirika pamoja na vyama vya ushirika wa akiba na mikopo (SACCOS), tutapata taarifa na wajumbe wa kamati ya siasa watajiridhisha na namna vinavyoendeshwa.

“Tunachosubiri sasa ni barua ya Ofisa Ushirika wa Wilaya na ratiba ya ziara nzima. Tumeshazungumza na Mkurungenzi Mtendaji wa Halmashauri yetu, Upendo Mangali, kumueleza kwamba tutazunguka na ofisa wake huyo kwa wiki moja hivi.

“Tutatembelea wilaya nzima, tuone, tupate hizo taarifa za vyama vyote kama nilivyosema ya vyama vya msingi na vyama vya ushirika na SACCOS.”

Katika hatua nyingine, juzi wakati wa kikao cha kamati ya ushauri ya wilaya hiyo, Mwenezi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Robert Mrisho, aliibua madai kuwa wilaya hiyo kwa sasa ina uhaba mkubwa wa maofisa watendaji wa vijiji.

Habari Kubwa