Hospitali ya Mawezi yanivunia kumaliza vifo vya uzazi

27Jan 2020
Mary Geofrey
KILIMANJARO
Nipashe
Hospitali ya Mawezi yanivunia kumaliza vifo vya uzazi

HOSPITALI ya Rufaa Mkoani Kilimanjaro ya Mawenzi, inajivunia kudhibiti vifo vitokanavyo na uzazi katika kipindi cha miaka miwili mfululizo bila kuwa na kifo cha mama.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mawezi, Dk. Jumanne Karia akifafanua jambo kwa waandishi wa habari hawapo pichani.

Mafanikio hayo, yameelezwa na Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk. Jumanne Karia, wakati akizungumza na waandishi wa habari, wakati wa ziara ya maofisa mawasiliano wa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, katika kampeni maalum ya 'Tumeboresha Sekta ya Afya'.

Lengo la kampeni hiyo ni kuangazia mafanikio ya miaka nne ya Serikali katika sekta ya afya.

Anasema katika kipindi cha miaka miwili hakuna kifo cha mama kilichotokea kutokana ubora wa huduma wanazotoa za kuhakikisha mama na mtoto wanakuwa salama.

Anasema mwaka jana jumla ya wanawake 3,411 walijifungua na walirudi nyumbani wakiwa salama na wenye afya.

"Haya ni mafanikio tunajivunia kama hospitali ya kuhakikisha tunapunguza na kumaliza vifo vitokanavyo na uzazi. Lengo ni kutoa huduma nzuri za kuwafanya kina mama kuona hii ni sehemu ya kuja kujifungulia," anasema Dk. Karia.

Jengo la mama na mtoto likiwa bado katika hatua za ujenzi katika hospitali ya Mawenzi.

Anasema mafaniko hayo yametokana na kutoa huduma za mkoba katika vituo vya kutolea huduma za afya kwenye halmashauri mkoani humo.

Anasema pia katika kipindi cha awamu ya tano wamefanikiwa kuajiri watumishi 40 wa kada mbalimbali kwa mwaka 2018/19.

"Tunaendekea kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi kwa kuwaendeleza kitaaluma pamoja na kulipa stahiki mbalimbali za watumishi," anasema Dk. Karia.

Anasema pia Serikali inaendelea na dhima yake ya kuendelea na ukamilishaji wa jengo jipya la mama na mtoto ambalo lipo kwenye awamu saba ya ujenzi.

Anasema Sh. bilioni 1.7 zimetolewa na Serikali kwa ajili ya hatua saba za ujenzi wake wote.

Sambamba na hilo anaelezea mafanikio mengine wanayojivunia kuwa ni kufanya upasuaji wa kuondoa ukungu kwenye lenzi ya jicho kwa wagonjwa 640.

Anasema pia wamepandikiza kioo cha jicho na huduma ya mkoba kwa ajili ya kuondoa ukungu kwenye lenzi ya jicho kwa wagonjwa 430.

Habari Kubwa