Hospitali Dar kukusanya damu zenyewe

07Feb 2016
Nipashe Jumapili
Hospitali Dar kukusanya damu zenyewe

HOSPITALI za Mwananyamala na Palestina zilizopo wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, katika kukabiliana na upungufu wa damu huku mahitaji yakiwa ni makubwa, zimeamua kuanzisha vituo vyake vya ukusanyaji.

Kaimu Mganga Mkuu wa Manispaa ya Kinondoni, Dk. Ezra Ngereza, aliliambia Nipashe uzinduzi wa vituo hivyo utafanyika kesho. Alisema wameamua kuwa na vituo katika hospitali hizo ili kukabiliana na tatizo la upungufu wa damu. Dk. Ngereza alisema mahitaji ya damu katika hospitali hizo ni makubwa huku usambaji ukiwa haujitoshelezi. “Mkakati ni kuanzisha vituo vya ukusanyaji damu katika hospitali hizi mbili ambapo wananchi watajitolea damu kwa hiari wakati wote na zitatumika moja kwa moja hospitalini baada ya sampuli zake kuhakikiwa usalama wake maabara ya damu salama,” alisema. “Tunaomba mara baada ya kuzinduliwa vituo hivi wananchi wajitokeze kuchangia damu kwa sababu uhitaji ni mkubwa hasa kutokana na ongezeko la watu,” alisema.

Habari Kubwa