Hoteli, vituo vya mafuta waliokaidi kulipa tozo ya maji kukiona

22Oct 2019
Frank Monyo
Dar es Salaam
Nipashe
Hoteli, vituo vya mafuta waliokaidi kulipa tozo ya maji kukiona

BODI ya Maji Bonde la Wami/Ruvu imesema itawapeleka mahakamani wamiliki wa Hoteli 73, Makampuni 13 na Vituo vya Mafuta 14 ambao wamekaidi kulipa ada ya mwaka ya watumia maji ya visima jumla ya shilingi milioni 328,530,00.

Afisa wa Bonde la Wami/ Ruvu Simon Ngonyani akizungumza na waandishi wa habari kulia ni afisa wa bonde hilo Harold Kayoza.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti  22, 2019 Jijini Dar es Salaam, Afisa wa Bonde la Wami/ Ruvu Simon Ngonyani, amesema kuwa ofisi yake imetoa notisi ya madai kwa wamiliki hao 100 ambapo baadhi yao walilipa jumla ya shilingi milioni 49,230,00.

Ametaja waliopeleka mahakamani kuwa ni Dar self Hotel, Mapumziko Hoteli,G&P Hoteli, Simba Oil, Manyangwe Hotel, Iceland Hoteli na Lunch time Hoteli.

“Tulikuwa na jitihada za kuwatafuta watu ambao walikuwa hawalipi ada za matumizi ya maji ya visima na wapo wachache ambao tumewapeleka mahakamani kwa kukahidi takwa la kisheria la kulipa ada za watumia maji ya visima na wakalipa huku wengine wakiahidi kulipa pasipo utekelezaji.,” amesema Ngonyani

Amezitaja baadhi ya Hoteli ambazo zinadaiwa kuwa ni BnB Hoteli, Confidence Hoteli, Don Lodge na Grand Villa Hotel, na kwa upande wa vituo vya mafuta ni TSN Oil, Gapco (T) LTD, Mantrac (T) LTD na Lake Group (Lake Oil) zote za Dar es Salaam.

Ngonyani ametoa tahadhari kwa wamiliki wa Hotel, Kampuni na vituo vya mafuta kuwa katazo la Waziri wa Maji Profesa Makame Mbarawa juu ya wamiliki wa visima vya majumbani kutolipa ada ya mwaka haiwahusu wao.

“Kumekua na sintofahamu baada ya tamko la Serikali mwaka huu juu ya kufuta tozo za matumizi ya maji ya visima majumbani hivyo kusababisha watumia maji kukaidi ulipaji wa tozo za maji za visima.,” alisema Ngonyani na kuongeza kuwa

“Tozo iliyofutwa ni ada za mwaka za matumizi ya maji ya visima majumbani iliyokua shilingi 100,000/=kwa mwaka kwa kila kisima kwa shughuli za nyumbani tu na sio kuuza maji. Aidha, tozo zinazotakiwa kulipwa kwa matumizi ya nyumbani ni; gharama za usajili wa kisima shilingi 60,000/=, gharama za kuomba kibali ya kuchimba kisima 150,000/= .,” amesema Ngonyani

Ameongeza kuwa kwa mteja ambae bado hajachimba kisima na gharama za upimaji wa ubora wa maji ni shilingi 241,000/= na mteja yeyote mwenye biashara kama Hoteli, Vituo vya mafuta, Nyumba za kulala wageni (Guest houses), viwanda na anatumia maji ya kisima ni lazima alipe tozo za maji za mwaka.

Amefafanua kuwa Sheria ya Usimamizi wa rasilimali za maji inasisitiza usajili wa visima ili kupata takwimu na taarifa zitakazosaidia katika ufuatiliaji wa mwenendo wa maji ardhini.

Amesema kuwa ulipaji wa ada hizo ni muhimu kwani husaidia bodi kuweza kutekeleza shughuli za utunzaji wa rasilimalli za maji zitakazo hakikisha upatikanaji wa maji kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi na kutimiza azma ya Rais Magufuli ya nchi kufikia uchumi wa viwanda.

Ameongeza kuwa ulipaji wa ada za matumizi mbalimbali ya maji ni takwa la kisheria kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Rasilimali za Maji Na.11 ya mwaka 2009 kifungu cha 43 (1) ambacho kinamtaka mtu yeyote anayetaka kuchepusha, kukinga, kuhifadhi, kuchukua na kutumia maji kutoka kwenye chanzo cha maji juu ya ardhi au chini ya ardhi au kujenga miundombinu yoyote lazima aombe kibali cha kutumia maji

"Sisi kama wataalamu tunawashauri kwamba bado wafuate utaratibu kwani kuchimba visima kiholelea si jambo zuri kwa afya zao hata kama wakichimba hawalipi lakini hii ya kutolipa haiwaondolei kwamba ni salama waje waombe vibali ili tuweze kufahamu nani anachimba wapi kwa sababu vinginevyo tutachimba hadi kwenye mashimo ya choo na matokeo yake ni hatari kwa afya zao pia," amesema Ngonyani

Amesema kuwa watu ambao wanachimba visima kiholela hasa kipindi hiki cha mvua wanakuwa katika hatari za kupata magojwa ya mlipuko kwani uchafu unaosombwa na maji ya mvua unaweza kupelekwa hadi kwenye visima kutokana na kutochimbwa kitaalamu.

Habari Kubwa