Huduma magonjwa ya dharura bado kikwazo

23Oct 2019
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe
Huduma magonjwa ya dharura bado kikwazo

MKUU wa Kitengo cha Magonjwa ya Dharura katika Hospitali ya Aga Khan, Dk. Sherin Kassamali, amesema bado kuna changamoto ya wataalamu wa kuhudumia wagonjwa wa dharura ikiwamo moyo kuacha kudunda ghafla.

Kassamali ambaye ni daktari bingwa wa magonjwa ya dharura, alisema jana kuwa kutokana na changamoto hiyo, hospitali hiyo kiithibati imekuwa kituo cha mafunzo maalum ya magonjwa ya dharura kutoka Taasisi ya Kimataifa ya Moyo ya Marekani (AHA).

Dk. Kassamali alisema ili kukabiliana na changamoto hiyo, hospitali hiyo imeamua kutoa mafunzo ya muda mfupi kwa wataalamu wa afya hospitali za serikali, binafsi na wadau wengine ili kukabiliana na matatizo hayo Tanzania.

Alisema matatizo moyo kuacha kudunda ghafla huweza kumtokea mtu muda na wakati wowote.

"Kwa mujibu wa AHA, takriban asilimia 90 ya watu wanaopata matatizo ya moyo kuacha kudunda ghafla, hufa wakiwa hawako chini ya uangalizi wa wataalamu hospitalini.

"Kituo hiki cha mafunzo kinawafundisha nini cha kufanya wakati moyo ukiacha kudunda ghafla, unapoacha kudunda maana yake hakuna mzunguko wa damu katika mwili na usipokuwapo inamaanisha seli katika mwili zinakufa. Seli zikifa maana yake mtu anafariki dunia," alisema.

Dk. Kassamali alisema seli zinaonyesha kwamba endapo mtu amepata tatizo hilo na akapewa mapema huduma ya dharura kitaalamu, inaweza kumwezesha kuendelea kuishi.

"Wako walioletwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) na hapa Aga Khan wakiwa katika hali ya moyo kuacha kudunda wakapewa huduma ya dharura inavyotakiwa wakaondoka nyumbani na nafuu," alisema.

Mkuu wa Idara ya Biashara na Ubora wa Chama cha Watoa Huduma Binafsi za Afya Tanzania (APHFA), Denis Mosha, alisema uelewa wa magonjwa ya dharura au kuchukua hatua wakati wa matatizo hayo, umekuwa changamoto kwa hospitali nyingi na hata kama upo ni kwa kiwango kidogo.

"Si kwamba wataalamu wa magonjwa ya dharura hawana uelewa kabisa bali tunataka waendane na teknolojia ambayo imeletwa na taasisi hii ya AHA.

"Kunatofauti ya kusoma darasani na kufanya mafunzo kwa vitendo, tunahitaji kumwokoa mgonjwa kwa hiyo elimu hii itawasaidia zaidi waweze kuokoa wagonjwa wengi zaidi," alisema.

Habari Kubwa