Huduma msaada wa kisheria kesho 

03Dec 2017
Mary Geofrey
Nipashe Jumapili
Huduma msaada wa kisheria kesho 

WIZARA ya Katiba ya Sheria kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo, mashirika yasiyo ya kiserikali, wanatarajia kutoa msaada wa kisheria bure katika maeneo mbalimbali nchini.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Mashirika yanayotoa huduma ya Msaada wa Kisheria nchini (TANLAP), Christina Kamili, akijibu maswali ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana. Kulia ni Naibu Katibu Mkuu wizara ya Sheria, Amon Mpanju na Kaimu msajili msaada wa kisheria, Felistas Joseph. PICHA: HALIMA KAMBI

Wataanza kutoa huduma hiyo kesho hadi Desemba 8, mwaka huu, katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam ikiwa sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Msaada wa Kisheria nchini yenye kauli mbiu ‘Msaada wa Kisheria kwa Maendeleo ya Wananchi’.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Amon Mpanju, alisema mgeni rasmi atakuwa Waziri wa Wizara hiyo, Prof. Palamagamba Kabudi.

Alisema maadhimisho hayo pia yatafanyika katika kanda zote nchini na katika mikoa ya Arusha, Dodoma, Mwanza, Kigoma, Mtwara na  Rukwa.

“Lengo kuu la maadhimisho haya ni kutoa elimu kwa umma juu ya uwapo wa sheria ya msaada wa kisheria. Pia maadhimisho haya yatajikita katika utoaji wa huduma ya msaada wa kisheria kwa wananchi na kuwatembelea wale walioko katika vituo vya polisi na magerezani,” alisema Mpanju.

Pia alisema katika maadhimisho hayo, mawakili wa kujitegema na wasaidizi wa kisheria wataungana kutoa huduma ya msaada wa kisheria kwa jamii ili kuhakikisha jukumu la upatikanaji haki kwa wananchi linafanikiwa.

Mpanju aliwataka wananchi wote wanaohitaji msaada wa kisheria kujitokeza katika mikoa iliyoainishwa ili kupata huduma hiyo bure bila malipo.

“”Ni haki ya kila binadamu kama ambavyo imeelezwa bayana katika Ibara ya 13 ya Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977 inavyoeleza na serikali kupitia sheria ya msaada wa kisheria ya mwaka 2017,” alisema Mapanju.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Mashirika ya Kutoa Msaada wa Kisheria, Christina Kamili, alisema kwa sasa nchini kote kuna wasaidizi wa kisheria 4,500.

Alisema kwa mujibu wa takwimu za utafiti uliofanywa Oktoba mwaka 2016 hadi Septemba mwaka huu, jumla ya watu 800 wamejitokeza kupata msaada wa kisheria na kesi 44,000 zilisikilizwa.

Kamili alisema kati ya hizo, kesi 7,800 ziliripotiwa na mashirika ya kiraia yanayotoa msaada wa kisheria kwa jamii ambayo yapo 66 katika maeneo mbalimbali  nchini.