Hujuma hifadhini 

23Jan 2023
Renatha Msungu
DODOMA
Nipashe
Hujuma hifadhini 

MAKAMU wa Rais, Dk. Philip Mpango, amesema baadhi ya mahakimu, majaji na mawakili wanashiriki kuhujumu maeneo ya hifadhi kwa kupokea rushwa na kuathiri utoaji haki.

Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango (katikati), akishiriki matembezi ya kilomita tano ya uzinduzi wa Wiki ya Sheria yaliyofanyika jijini Dodoma jana. Kushoto kwake ni Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Juma. PICHA: IBRAHIM JOSEPH

Amesema hujuma hizo zinajumuisha mahakama kuzuia minada ya mifugo inayokamatwa kwenye maeneo hayo na  kuwatoza faini ndogo wamiliki wa mifugo.

Akizindua Wiki ya Sheria kwenye Viwanja vya Nyerere Square jijini hapo jana, Makamu wa Rais alisema: "Katika ziara zangu ninazofanya mikoani na nyingine zinanikuta ofisini, ninapokea malalamiko mengi ya wananchi kuhusu mhimili wa mahakama lakini na vyombo vingine - polisi na magereza yenyewe, kwenye mfumo wa utendaji na utoaji haki kwa ujumla wake.

"Baadhi ya malalamiko ninayosikia ni kwamba baadhi ya mahakimu, mawakili na majaji sio waaminifu, wanadai rushwa kinyume cha kiapo chao, kuna minada ya mifugo ambayo inakamatwa kwenye maeneo ya hifadhi, mara kadhaa Mbeya kule tunaletewa malalamiko minada hiyo inazuiliwa kwa amri ya mahakama.

"Tena wakati mwingine unashtuka kabisa hiyo mahakama inakaa Jumapili au basi hizo faini ambazo zinaamriwa ni ndogo mno, kwa hiyo mwenye mifugo yake analipa faini baada ya nusu saa anarudisha mifugo yake kwenye hifadhi."

Pia alisema amepokea malalamiko ya fedha za kigeni zinazokamatwa mipakani, zinapotea mikononi mwa mahakama na hukumu zinapindishwa ili kumpa ushindi mwenye fedha.

"Yapo malalamiko mengine, ni pamoja na gharama kubwa za uendeshaji wa kesi na kulipa gharama za mawakili, wananchi wanalalamikia hukumu kuandikwa kwa lugha ya Kiingereza lakini pia watuhumiwa wanakaa mahabusu muda mrefu wanasubiri uchunguzi kukamilika.

"Wananchi wengine wanasema 'jamani hatuna elimu ya sheria', hivyo kuna ukosefu wa elimu ya sheria kwa umma pamoja na jitihada zote ambazo mmefanya," alisema.

Aliwataka wahusika katika mfumo wa utoaji wa haki kuendelea kutoa elimu kwa umma na kuhakikisha huduma mbadala ya usuluhishi inapatikana na kufikika kwa urahisi.

"Nitoe wito kwa mahakama kushirikiana vyema na wadau katika kuimarisha utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi ili kufikia malengo yake kirahisi," aliagiza.

Makamu wa Rais alisema mawakili wa kujitegemea wanapaswa kujielekeza katika kutoa elimu na ushauri sahihi kwa wateja wao kuhusu namna bora ya kutatua migogoro ikiwa ni pamoja na kutumia njia mbadala ya usuluhishi badala ya kuendelea na kesi mahakamani.

"Asasi za kiraia na mashirika yasiyo ya kiserikali yaendelee kutoa elimu kwa umma, misaada kwa wananchi na kujenga uelewa kuhusu haki za msingi za kiraia na umuhimu wa utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi, pia viongozi wa dini na viongozi wa mila kote nchini wasaidie mahakama kuzungumza na wananchi kuhusu umuhimu wa utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi," alielekeza.

Pia aliagiza kuangaliwa upya ufanyaji kazi wa mabaraza ya ardhi nchini kutokana na kuongezeka kwa migogoro ya ardhi inayokosa usuluhishi wa mapema.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Hamis Juma, alitoa rai kwa wananchi wanaohitaji kudai haki zao, kufahamu kwanza haki hizo kwa kusoma na kutafuta elimu itakayowezesha kufahamu sheria na taratibu zinazoongoza haki inayotafutwa.

Alisema Wiki ya Sheria itatumika katika kutoa elimu na kuwakumbusha wananchi namna ya kupata haki zao kwa njia sahihi na rahisi.

Alisema wananchi wana wajibu wa kumaliza mashauri kwa njia ya usuluhishi huku akitoa wito kwa wananchi kutembelea Maonesho ya Wiki ya Sheria na hususani Mahakama Kuu Kituo cha Usuluhishi ili kupata elimu na uelewa zaidi kuhusu njia hiyo iliyosheheni faida lukuki kwa kuwa kufanya hivyo kutawapa nafasi ya kufanya shughuli za uzalishaji na kujiongezea kipato.

"Ni muhimu wananchi wafahamu pia namna ambavyo migogoro ya biashara, kazi au mikataba inayoweza kutokea kwa njia za mitandao," alisema.

Maonyesho hayo yaliyozinduliwa jana yatafanyika kwa siku nane hadi Januari 29 yatajapohitimishwa yakifuatwa na kilele cha Siku ya Sheria itakayofanyika Februari Mosi mwaka huu, Rais Samia Suluhu Hassan akiwa mgeni rasmi.

Habari Kubwa