Hukumu dhidi Mhadhiri UDSM matunzo ya watoto, Julai 29

19Jul 2021
Kulwa Mzee
Dar es Salaam
Nipashe
Hukumu dhidi Mhadhiri UDSM matunzo ya watoto, Julai 29

MAHAKAMA ya Watoto Kisutu inatarajia kutoa hukumu dhidi ya Mhadhiri Mwandamizi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Aviti Mushi na Getrude Mushi, wanaobishana matunzo ya watoto, Julai 29, mwaka huu.

Uamuzi huo wa mahakama umefikiwa baada ya Hakimu Devotha Msofe, kusikiliza malalamiko ya Getrude na majibu ya Dk. Aviti.

Mlalamikaji katika shauri hilo anadai wamefanikiwa kuzaa watoto wawili na mlalamikiwa ambao wanahitaji kupata matunzo kutoka kwa baba huyo.

Anadai kwa sasa watoto wako chini ya uhifadhi wa mama na mlalamikiwa anawajibika kutunza watoto wake, lakini tangu 2020 hajatoa matunzo ya aina yoyote ikiwamo ada.

Getrude anadai alipeleka taarifa Ustawi wa Jamii Mei, mwaka jana na Desemba 11 mwaka huo alikubali kutoa matunzo, lakini hakutekeleza.

Mlalamikaji anadai katika makubaliano alikubali kulipa ada za shule na atatoa Sh. 700,000 kwa mwezi.

Baada ya mlalamikiwa kukiuka makubaliano shauri hilo lilifikishwa mahakamani Juni 9, mwaka huu kwa faida ya watoto na limesikilizwa na kupangwa kwa ajili ya hukumu Julai 29, mwaka huu.

Habari Kubwa