Hukumu kesi wakala Richmond Aprili 21

11Mar 2017
Hellen Mwango
Dar es Salaam
Nipashe
Hukumu kesi wakala Richmond Aprili 21

HATIMAYE hukumu ya mfanyabiashara Naeem Gire anayekabiliwa na mashtaka ya kughushi nyaraka za uongo dhidi ya Kampuni hewa ya kufua umeme ya Richmond Development LLC, imepangwa kutolewa April 21, mwaka huu.

Uamuzi huo ulitolewa jana na Hakimu Mkazi Mkuu, Mfawidhi, Cyprian Mkeha anayesikiliza kesi hiyo katika Mahakama Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam.

Awali, Gire anayedaiwa kuwa wakala wa kampuni hewa ya kufua umeme wa dharura, Richmond Development LLC, anabiliwa na mashtaka ya kughushi, kutoa taarifa za uwongo na kuziwasilisha serikalini.

Awali, Julai 28, 2011, aliachiwa huru na Hakimu Mkazi Mkuu, Waliarwande Lema katika mahakama hiyo baada ya kumwona hana kesi ya kujibu baada ya upande wa Jamhuri kufunga ushahidi wake.

Hata hivyo, Mahakama Kuu Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, iliamuru kesi hiyo kusikilizwa ushahidi wa upande wa utetezi.
Katika kesi ya msingi, Gire anakabiliwa na mashtaka matatu ya kughushi nyaraka , kutoa taarifa za uwongo na kuwasilisha taarifa hizo za uwongo kuwa mitambo ya kuzalisha umeme ya ‘Richmond’ ina uwezo wa kufua megawati 100 za umeme, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Januari 14, 2010 Gire alifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza na kusomewa mashtaka matatu, ikiwamo kughushi nyaraka, kutoa taarifa za uwongo na kuwasilisha nyaraka za kughusi katika Kamati ya Zabuni ya Shirika la Umeme (Tanesco).

Ilidaiwa kuwa Machi 13, 2006 aligushi hati ya nguvu ya kisheria (Power of Attorney) akionesha kuwa Mwenyekiti wa kampuni ya Richmond Development LLC, ya Texas Marekani, Hamed Gire amempa mamlaka ya kusimamia shughuli za kampuni hiyo nchini Tanzania.

Shtaka jingine ilidaiwa kuwa Julai 20, 2006 aliwasilisha hati hiyo ya kughushi kwa Kamati ya Zabuni ya Tanesco, na kutoa taarifa za uwongo kwamba Richmond ina uwezo wa kuzalisha umeme wa Megawati 100, ili kuwashawishi wajumbe wa kamati hiyo wampe zabuni hiyo.

Habari Kubwa