Hukumu ya kina Mbowe Machi 10

25Feb 2020
Hellen Mwango
Dar es Salaam
Nipashe
Hukumu ya kina Mbowe Machi 10

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam imepanga Machi 10, mwaka huu, kutoa hukumu ya vigogo tisa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) akiwamo Mwenyekiti Taifa, Freeman Mbowe na wenzake wanane na kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Vincent Mashinji wanaokabiliwa na ...

kesi ya uchochezi.

Uamuzi huo ulitolewa jana na mahakama hiyo iliyoketi chini ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.

Mbali na Mbowe na Mashinji, wengine ni, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu; Katibu Mkuu Chadema na Mbunge wa Kibamba, John Mnyika; Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa; Mbunge wa Tarime Mjini, Ester Matiko; Mbunge wa Kawe, Halima Mdee; Mbunge wa Bunda, Ester Bulaya na Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche.

Hakimu Simba alisema sheria inaelekeza pande zote mbili Jamhuri na utetezi kufanya majumuisho ya mwisho ili kuisaidia mahakama kutoa uamuzi kwa kuangalia masuala ya kisheria yaliyoibuliwa wakati wa usikilizaji wa kesi hiyo.

Alisema wametoa maelekezo kwa pande zote kuwasilisha hoja zao baada ya mahakama kukamilisha uchapaji wa nyaraka zilizopo kwenye kesi hiyo na kuwagawia mawakili wa pande zote.

"Kesi hii inamvuto kwa jamii ni lazima iishe ili kila mmoja aweze kuendelea na shughuli zake. Majumuisho ya mwisho mnatakiwa muyawasilishe siku tano za kazi, kwa njia ya maandishi, mwenendo wa kesi hii una kurasa zaidi ya 1,000 ambazo natakiwa kupitia na kutoa hukumu, hivyo hukumu ya kesi hii itatolewa Machi 10, mwaka huu asubuhi," alisema Hakimu Simba.

MDEE AMPUUZA MASHINJI

Kabla ya kesi hiyo kuanza, Dk. Mashinji alikutana na viongozi wa Chadema ikiwa ni siku chache tangu alipohamia CCM.

Awali, mahakamani hapo Dk. Mashinji ambaye alifika na kuanza kusalimiana na viongozi mbalimbali wa Chadema wakiwamo washtakiwa wenzake, Mdee alikataa kupokea mkono, huku akiendelea kuchezea simu yake ya mkononi kama vile hakuna mtu mbele yake.

Aidha, washtakiwa hao walionekana kumtenga Dk. Mashinji, hivyo kubaki peke yake tofauti na ilivyokuwa awali kabla hajahamia CCM.

Upande wa Jamhuri katika kesi hiyo uliita mashahidi wanane na mahakama iliwaona washtakiwa wote kuwa na kesi ya kujibu, kujitetea pamoja na kuleta mashahidi wanne.

Mwaka 2018, viongozi hao walifikishwa mahakamani hapo wakikabiliwa na mashtaka 13 likiwamo la kufanya mkusanyiko usiohalali uliosababisha kifo cha mwanafunzi wa Chuo cha Usafirishaji cha Taifa (NIT), Akwilina Akwiline.

Akisoma mashtaka hayo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Faraja Nchimbi alidai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri (sasa Jaji wa Mahakama Kuu), kuwa washtakiwa kwa pamoja walitenda makosa hayo Februari 16, mwaka huo maeneo ya Viwanja vya Buibui pamoja na barabara ya Kawawa Mkwajuni wilayani Kinondoni, Dar es Salaam.

Katika mashtaka ya kwanza la kula njama, kwa pamoja inadaiwa Februari Mosi na 16, 2018, Dar es Salaam walikula njama pamoja na wenzao ambao hawapo mahakamani walikula njama ya kutenda kosa la kufanya mkusanyiko usio halali, mkusanyiko wenye ghasia na kukiuka tamko kutawanyika.

Ilidaiwa pia Februari 16,2018 katika viwanja vya Buibui na Mwananyamala Kinondoni washtakiwa hao wakiwa wamekusanyika na azima ya pamoja, waliitekeleza kwa kufanya mkusanyiko usio halali na kusababisha watu waogope kuwa watakwenda kupelekea uvunjïfu wa amani.

Kadhalika washtakiwa hao wanadaiwa kuwa Februari 16,2018 walifanya mkusanyiko wenye ghasia, wanadaiwa kuwa siku hiyo katika viwanja vya Buibui Mwananyamala na barabara ya Kawawa Kinondoni kwa pamoja na wenzao 12 ambao hawapo mahakamani walitekeleza mkusanyiko ama maandamano yasiyo halali wakiwa na lengo la kuvamia ofisi ya mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni na kuĺeta hofu ya uvunjifu wa amani.

Nchimbi alidai kuwa Februari 16, 2018 katika barabara ya Kawawa Kinondoni Mkwajuni washtakiwa hao wakiwa na wenzao 12 ambao hawapo mahakamani walikiuka tamko la kuwataka kutawanyika la Ofisa wa Polisi, SSP Gerald Ngiichi kwa kugoma kutawanyika na kupelekea uvunjifu wa amani ambao ulisababisha hofu na hatimaye kifo cha Akwilina na majeruhi kwa askari wawili ambao ni Konstebo Fikiri na Koplo Rahim Msangi.

Habari Kubwa